Na Tatu Mohamed, JamhuriMedia, Dodoma

NJIWA wa mapambo waliowasilishwa kwenye Maonesho ya Kimataifa ya Wakulima na Wafugaji (Nanenane) yanayoendelea jijini Dodoma wamegeuka kivutio kikubwa kwa wananchi kutokana na muonekano wao wa kipekee pamoja na bei yao.

Mfugaji wa njiwa hao, Abdulaziz Almasi, amesema ameleta aina 10 tofauti za njiwa wa mapambo, ambapo kila mmoja huuza kuanzia shilingi laki nne (400,000) hadi kufikia milioni moja (1,000,000).

“Watu wengi wanashangazwa na bei, lakini hizi ni aina za kipekee za njiwa wa mapambo. Wengine wanatoka Marekani na Ujerumani. Muonekano wao, umbile na asili yao ndio vinawafanya kuwa wa gharama,” amesema Almasi.

Ameeleza kuwa njiwa hao wanaweza kufugwa kwa malengo ya mapambo au kibiashara, na kwamba hula mtama, choloko na uwele, huku wakizaliana kwa wingi.

Almasi ambaye amejikita kwenye biashara hiyo kwa zaidi ya miaka 15, amesema alianza na njiwa sita tu, lakini hadi sasa anamiliki zaidi ya njiwa 2000 wa mapambo huku wakiwa wa aina zaidi ya 90.

Kwa mujibu wa Almasi, biashara hiyo ni fursa ambayo Watanzania wengi bado hawajaichangamkia kikamilifu, licha ya kuwa na soko la uhakika na faida kubwa endapo mfugaji atazingatia ubora na soko sahihi.

Banda lake limekuwa moja ya maeneo yanayovutia watu wengi kwenye maonesho hayo, ambapo baadhi ya waliotembelea wameonekana kushangazwa na uwepo wa njiwa wenye thamani inayofikia hadi milioni moja kwa mmoja.

Maonesho ya Nanenane mwaka huu yameendelea kuonyesha ubunifu wa sekta ya kilimo na mifugo, huku biashara ya njiwa wa mapambo ikiwa miongoni mwa maeneo yanayoibua mjadala mpya kuhusu kilimo mseto na uwekezaji wa aina tofauti vijijini na mijini.