
Mgombea urais kupitia chama cha NLD, Doyo Hassan, amesema chama chake kimeendesha kampeni za kistaarabu na kisayansi katika mikoa yote 26 nchini, akisisitiza dhamira ya serikali watakayoiongoza kuwa ya kumkomboa Mtanzania kiuchumi na kuwashauri kukichagua chama hicho ili kupata maendeleo.
Akizungumza leo Octoba 16,2025 jijini Dar es Salaam katika moja ya mikutano ya kampeni, Doyo amesema ilani ya chama hicho imeweka vipaumbele vinavyojikita katika kumwezesha kijana kujiajiri, kujitegemea na kuchochea ukuaji wa uchumi wa wananchi wa kipato cha chini.
“Ilani yetu imeeleza wazi namna tutakavyomsadia Mtanzania kujikwamua kiuchumi. Tunataka kuona kijana anaajiriwa, anajiajiri na kuacha utegemezi. Nawaomba Oktoba 29 mjitokeze kupiga kura, mnichague ili niweze kuinyoosha nchi yetu,” alisema Doyo.
Aidha, Doyo amewataka wananchi kuhakikisha uchaguzi unafanyika kwa amani ili kuepuka vurugu zinazoweza kuathiri maendeleo ya taifa.

Aidha Doyo ameahidi kupunguza gharama zisizo za lazima ikiwemo misafara mikubwa ya Rais, akisema fedha hizo zitapelekwa kwenye miradi ya maendeleo ya wananchi.
Kwa upande wake, Gradiness Msuya, mgombea ubunge wa jimbo la Ubungo, amewataka wananchi kuhakikisha hawafanyi makosa siku ya kupiga kura ili kuleta mabadiliko chanya kwa maendeleo ya jimbo hilo.
“Niwaombe tarehe 29 msifanye makosa. Tukiungana tutaleta mageuzi katika nchi yetu, lakini pia tuijenge Ubungo yetu,” amesema Msuya.
Naye Mkurugenzi wa kampeni za chama hicho, Ibrahim Pogola, amesema NLD imeanzisha mbinu mpya ya “mobile kampeni” ambapo wanawafuata wapiga kura walipo badala ya kutumia mikutano mikubwa yenye gharama.

“Tunafanya kampeni za kisayansi. Hatuleti wasanii wala kubeba wananchi kwa magari. Tunawafuata wananchi walipo ili tusikilize matatizo yao na tuwaeleze sera zetu moja kwa moja ili wao wafanye maamuzi” amesema Pogola.
Amesisitiza kuwa ilani ya NLD imelenga kupunguza maslahi makubwa ya wabunge na kuelekeza fedha hizo kuboresha mishahara ya walimu na madaktari.


