Benki ya NMB imeendeleza jitihada zake za kujenga nguvu kazi yenye ujuzi na maarifa ya kisasa katika sekta ya fedha nchini kwa kusaidia mafunzo ya kitaaluma na kutalaamu kwa vijana 100 kupitia mpango maalumu wa mafunzo ya Graduate Banker Readiness Programme (GBRP) katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
Kupitia mpango huo, Benki ya NMB kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, inatoa mafunzo, maarifa ya vitendo, na ufaham wa kina wa sekta ya fedha. Kundi la nne la mpango huu, kama ilivyokuwa kwa makundi yaliyotangulia, limepata mafunzo ya ujuzi muhimu, maarifa ya vitendo, na ufahamu wa kina wa sekta ya fedha, na lilihitimu Ijumaa iliyopita.
Akizungumza kabla ya kuwakabidhi wahitimu vyeti, Mkuu wa Idara ya Rasilimali watu wa Benki ya NMB, Bi. Erica Hanson, alisema mpango huu ni matokeo ya ushirikiano wa kimkakati kati ya Benkiy a NMB na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, kupitia shule ya Biashara ya Chuo hicho, ukiwa na lengo la kuunganisha elimu ya darasani na uhalisia wa kazi za benki.
Bi Erica alibainisha pia kuwa washiriki wamepata mafunzo ya kutosha katika maeneo kadhaa ya msingi ikiwemo uchambuzi wa kifedha, uendeshaji wa benki, usimamizi na udhibiti wa vihatarishi, uzingatiaji wa kanuni, utoaji bora wa huduma kwa wateja, na mifumo ya benki ya kidijitali.
“Kuhitimu kwa vijana hawa leo pia kunaongeza nguvu katika dhamira ya NMB ya kuendelea kujijenga kama mwajiri pendwa nchini, jambo ambalo limethibitishwa kwa kutunukiwa Tuzo ya Mwajiri Bora kwa miaka mitatu mfululizo. Haya yote ni matokeo ya uwekezaji wa makusudi katika watu, vipaji na maendeleo endelevu ya rasilimali watu.” aliongeza Bi Hanson.
Kwa upande wa wanataaluma kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam wakiongozwa na Mkuu wa Kitivo cha Biashara wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Prof. Omari Mbura, walisema kuwa mpango huu unasaidia kupunguza pengo la ujuzi sokoni, kuhakikisha wahitimu wanakidhi mahitaji halisi ya tasnia. Maneno hayo pia yaliakisiwa na hotuba zilizotolewa na Mratibu wa mafunzo hayo, yaliyoandaliwa na Kituo cha Utafiti wa Benki na Huduma za Kifedha (CBFSR), Prof. Esther Ishengoma na Dkt Thobias Swai, Mkuu wa Idara ya Fedha ambao walizungumza kwa nyakati tofuati.
Marcelina Evarist, aliyezungumza kwa niaba ya wahitimu, aliishukuru benki ya NMB kwa kuuwezesha mpango huo kabambe uliowajengea uwezo na kuongeza ufahamu wao kuhusu sekta ya fedha.





