Na Mwandishi Wetu,JamhuriMedia, Dodoma
BENKI ya NMB imekabidhi Sh100 Milioni kwa Wizara ya Kilimo ili kusaidia kwenye maandalizi ya maonyesho wakulima, wafugaji na wavuvi maarufu kama nanenane.
Kiasi hicho ni sehemu ya jumla ya Sh470 milioni ambazo NMB imefadhili kwa maonyesho hayo katika kipindi cha miaka saba.
Akizungumza wakati wa makabidhiano ya fedha hizo, Meneja wa NMB Kanda ya kati Janeth Shango amesema wataendelea kufadhili shughuli za kuimarisha kilimo na ufugaji ili kiwe cha tija zaidi kwa wakulima, wafugaji ili kuimarisha uchumi wa kitaifa.
Shango amesema fedha hizo zinatolewa Wizarani ili ziende kuwagusa wakulima moja kwa moja na kuwainua kiuchumi.
“Siyo mara ya kwanza kuungana na wakulima, wafugaji na wavuvi, benki hii kupitia NMB Foundation hadi sasa tumeshawafikia vyama vya Ushirika na Amcos zaidi ya 1500 kwa wakulima wa kahawa,Ufuta,Tumbaku na Korosho,”amesema Shango.
Meneja amesema ili Taifa liweze kuimarika lazima watu wake waimarike kifedha na ndiyo maana wanapeleka uwezeshaji kwa walengwa wenyewe.
Hata hivyo amesema NMB inalenga kuwatoa wakulima katika Kilimo cha mazoea kwenda katika Kilimo cha kisasa ambacho kitawakomboa katika ulimwengu wa sasa.
Mkuu wa idara ya Kilimo Biashara benki ya NMB, Nsolo Mlozi amesema ndani ya benki hiyo wamekuwa na utamaduni wa kutengeneza kalenda maalum kulingana na misimu ya Kilimo ambayo hulenga kuwafanya wakulima wafurahie matunda ya jasho lao.
Mlozi amesema NMB ipo kwenye mkakati wa kuwatoa wakulima katika Kilimo cha kutegemea mvua ili wahamie kwenye umwagiliaji.
Mbali na hilo ameelezea fursa mojawapo ni kuwaunganisha wakulima na masoko ya Kimataifa kupitia benki rafiki na NMB Duniani lakini akisisitiza wakulima kuwa na Bima za mazao.
Akipokea hundi ya msaada huo, Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Gerald Mweri amesema fedha hizo zitakuwa msaada mkubwa katika maandalizi yao kwenye maonyesho hayo ambayo yanashirikisha zaidi ya washiriki 500.
Mweri amesema Sh100 milioni ni kiasi kikubwa ambacho si kuwafikia wakulima pekee katika maonyesha bali Wizara itafanya maboresho makubwa kwenye Miundombinu yake inayohusiana na maonyesho.
Amekiri kuwa benki hiyo imekuwa rafiki na ndugu kwao hivyo akaomba wawe sehemu ya washiriki katika maonyesha ya Kitaifa Nzuguni (Dodoma) na yale ya Kanda ambayo yatakuwa katika Mikoa ya Arusha, Morogoro, Simiyu na Mbeya ambako sehemu zote zitakuwa na watu wenye kuhitaji huduma za NMB



