Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Arusha
Kutokana na kuongezeka kwa magonjwa yasiyoambukiza nchini ambayo yanaendelea kuathiri nguvu kazi ya Taifa kwa kushambulia watu wa rika mbalimbali, Watanzania wameshauriwa kujenga utamaduni wa kupima afya zao mara kwa mara na kuzingatia kanuni bora zenye usalama wa afya zao.
Rai hiyo imetolewa jana jijini Arusha na Mkurugenzo Mtendaji wa Kampuni ya Norland Global Tanzania, Dk. Moses Makalla, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu namna bora ya watu kulinda afya zao ili waweze kushiriki vema katika shughuli za kijamii na kiuchumi.
“Ni muhimu kuchukua hatua madhubuti za kukabiliana na magonjwa yasiyoambukiza kwa kuwa dalili zake mara nyingi hazijitokezi mapema. Hivyo, kupima afya mara kwa mara ni hatua muhimu ya kujikinga kabla ya kushambuliwa na maradhi hayo,” amesema Dk. Makalla.
Ameeleza kuwa Norland Global ni kampuni inayojihusisha na utafiti, utengenezaji na utoaji wa tiba kwa magonjwa mbalimbali yasiyoambukiza yenye makao makuu nchini China, huku ikitoa huduma za matibabu duniani kote kwa kutumia bidhaa za asili zilizofanyiwa tafiti za kina na kuthibitishwa na taasisi za afya za kitaifa na kimataifa.
Kwa mujibu wa takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO) za mwaka 2020, magonjwa yasiyoambukiza yalichangia zaidi ya vifo milioni 41, sawa na asilimia 71 ya vifo vyote duniani, ikilinganishwa na vifo milioni 57 vilivyoripotiwa mwaka 2016. Nchini Tanzania, magonjwa hayo yanachangia takribani asilimia 33 ya vifo vyote.
Aidha, takwimu za hivi karibuni kutoka Wizara ya Afya zinaonesha ongezeko kubwa la magonjwa hayo, ambapo katika kipindi cha Julai 2022 hadi Machi 2023, magonjwa yasiyoambukiza yaliyopelekea wagonjwa wengi kuhudhuria vituo vya afya ni pamoja na shinikizo la juu la damu, ambapo wagonjwa 1,456,881 waliripotiwa sawa na asilimia 49, ikilinganishwa na asilimia 34 katika kipindi kama hicho cha mwaka 2021/2022.
Kisukari kiliripotiwa kwa wagonjwa 713,057 sawa na asilimia 24, huku magonjwa ya mfumo wa hewa yakihusisha wagonjwa 386,018 sawa na asilimia 13, ikilinganishwa na asilimia 10 katika kipindi kama hicho cha mwaka uliotangulia.
Dk. Makalla amesema tafiti za miaka ya 1986/1987 zilionesha kuwa mtu mmoja pekee ndiye aliyekuwa na ugonjwa wa kisukari, huku watu watano wakibainika kuwa na shinikizo la juu la damu, hali inayoonesha ukubwa wa ongezeko la magonjwa hayo kwa sasa.
Amefafanua kuwa kwa sasa magonjwa hayo yameongezeka kwa wastani wa ,mara tano hadi tisa ikilinganishwa na miaka ya 1980, ambapo wakati huo ni asilimia moja pekee ya Watanzania waliokuwa na kisukari na asilimia tano wakiwa na shinikizo la juu la damu, tofauti na sasa ambapo kisukari kimefikia asilimia 9 na shinikizo la juu la damu asilimia 25.
“Malengo yetu makubwa kwa mwaka huu mpya wa 2026 ni kuunga mkono jitihada za Serikali na Wizara ya Afya katika mapambano dhidi ya magonjwa yasiyoambukiza, ili kuokoa nguvu kazi ya Taifa ambayo inaweza kuathirika kutokana na ukosefu wa matibabu sahihi,” alibainisha.
Amesema magonjwa yanayowaathiri Watanzania wengi ni pamoja na kisukari, shinikizo la juu la damu, magonjwa ya figo, homa za ini, upungufu wa damu, tindikali tumboni (acid reflux) pamoja na vidonda vya tumbo.
Aidha, magonjwa mengine ni pamoja na aina mbalimbali za saratani ikiwemo saratani ya shingo ya kizazi na ya matiti kwa wanawake, saratani ya tezi dume kwa wanaume, pamoja na saratani ya ngozi, damu na utumbo.
“Nitumie fursa hii kuwahimiza Watanzania kutumia tiba za Norland Global ambazo zimeonesha mafanikio makubwa katika kusaidia kukabiliana na changamoto hizi za kiafya,” alisisitiza Dk. Makalla.

