-Mamia wamsindikiza kwa ngoma, vifijo na nderemo

-Aaahidi kushirikiana na watia nia wote kuijenga Nyasa

-Awataka Wananchi kuunga mkono juhudi za kuleta maendeleo

Na Byarugaba Innocent, Nyasa DC

Mapema leo Agosti 26, 2025 mgombea Ubunge Jimbo la Nyasa kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) John John Nchimbi amefika mbele ya Ofisi ya msimamizi wa Uchaguzi Jimbo ambapo mara baada ya kujitambulisha kwa barua kutoka tume huru ya Uchaguzi alikabidhiwa rasmi fomu na ndugu Ausi Mkwanda Limia tayari kwenda kunadi sera kwa wananchi kuomba ridhaa ya kuliongoza Jimbo la Nyasa kwa kipindi cha miaka mitano.

Nchimbi ameisimamisha Nyasa kwa muda ambapo mamia ya wananchi wanawake kwa wanaume wa rika tofauti walijitokeza kumsindikiza huku msafara ukiongozwa msululu mrefu wa ‘bodaboda’Bajaji,Magari ukipambwa na vigoma vikipiga nyimbo za kumpongeza kwa kuteuliwa na kuwa mgombea atakayewawakilisha kwenye Jimbo hilo.

Awali Mwenyekiti wa CCM Wilaya Abel Komba kabla ya kumkaribisha mgombea kuwasalimia wananchi aliishukuru tume huru ya Uchaguzi kwa maandalizi na mapokezi mazuri waliyoyapata tangu walipofika na mgombea kuchukua fomu kwa Maelekezo na miongozo inayotakiwa.

Kwa upande wake Nchimbi amewashukuru wananchi kwa Upendo,Mahaba na mshikamano mkubwa waliomwonesha na kwamba hiyo ni heshima na deni kubwa kwake wakati wa Utumishi

Akiongea kwa sauti ya upole na unyenyekevu mkubwa,Nchimbi amewashukuru watia nia wote waliokuwa kwenye kinyang’anyilo cha kupewa ridhaa ya kuliongoza Jimbo la Nyasa kwa ustaarabu walioonesha kipindi chote cha mchakato kwani kampeni zilifanyika kindugu na yeye yupo tayari kushirikiana nao kwa Maendeleo ya Jimbo la Nyasa.

Nchimbi amesema kuwa kando ya kupata asilimia 90 ya ushindi kwenye kura za Maoni, anatamani kupata mchango wa asilimia 5-10 alizozikosa huku akikemea tabia za wanasiasa wengine ambao huwanyooshea vidole wanaokuwa tofauti nao kimtazamo

“Twendeni tukawatafute wenzetu wasiokuwa na amani ili tuwape amani,tushikane mikono, twende pamoja kuijenga Nyasa yetu”ameongeza Nchimbi.

Jumla ya wagombea watano tayari wamechukua fomu za kugombea Ubunge Jimbo la Nyasa mwingine ni John Gouttman Ndimbo kupitia Chama Cha ACT-Wazalendo,Jenifa Hurbani Mbele-UDP, Goodluck Patrick Sangana-CHAMA CHA MAKINI na Omary Cosmas Makukula-CCK.