Na Stella Aron, JamhuriMedia, Tanga

Mabadiliko ya tabianchi huathiri nyasi bahari kwa njia mbalimbali lakini pia nyasi bahari huaribiwa na shughuli za kibinadumu.

Muonekano wa bustani za nyasi baharini unaweza usiwe wa kupendeza kama miamba ya matumbawe au kama misitu ya mikoko, lakini ni maficho ya samaki, hulinda ukanda wa pwani kutokana na dhoruba na ni hifadhi kuu za kaboni, na ni baadhi ya maeneo ya asili yenye thamani zaidi duniani.

Licha ya umuhimu wa nyasi hizo, mifumo hii ya ikolojia iko hatarini.Kwa ulinganifu, ni sawa na kusema uwanja wa mpira wa nyasi baharini hupotea kila baada ya dakika 30 na inakadiriwa asilimia 7 ya malisho hupotea ulimwenguni kote kwa mwaka.

Asidi ya bahari, maendeleo ya pwani na kupanda kwa joto la bahari kutokana na mabadiliko ya tabianchi ni vichochezi vikuu vya upotevu wa nyasi baharini.

Ili kuongeza ufahamu kuhusu hatari iliyopo kwa mifumo hii ya ikolojia, Shirika la Kimataifa la Uhifadhi wa Mazingira na Uasilia (IUCN) ambao wanatekeleza mradi wa Bahari Mali kwa kushirikiana na Chama cha Waandishi wa Habari za Mazingira Tanzania (JET), wametoa mafunzo kwa waandishi wa habari wa mazingira yaliyofanyika mkoani Tanga.

IUCN hutoa msaada wa kifedha na mafunzo ya kiufundi kwa kipindi cha mwaka mmoja na baadaye jamii huhimizwa kusimamia urejeshaji huo kwa kujitegemea huku wakiendelea kufuatiliwa na kupatiwa ushauri.

Joseph Olilla ni Meneja wa Mpango wa Ustahimilivu wa Pwani na Bahari, Shirika la Kimataifa la Uhifadhi wa Mazingira na Uasilia (IUCN), anasema urejeshwaji huo ni sehemu ya mradi wa Bahari Mali unaotekelezwa katika mikoa ya Pemba na Tanga unaolenga kutumia fursa ya uchumi wa buluu kwa njia jumuishi na endelevu kulinda bayoanuwai ya pwani na baharini.

Kupitia mradi huo waliwezesha kurejeshwa hekari 90.4 za mikoko katika wilaya katika wilaya za Mkinga na Pangani mkoani Tanga na wilaya za Mkoani na Michenzani kisiwani Pemba ndani ya miaka mitatu. Anasema urejeshwaji huo unafanywa na jamii wakiongozwa na maofisa wa serikali huku wao wakitoa msaada wa kifedha na mafunzo.

Nyasi bahari ni mimea ya kijani inayoota chini ya bahari (kwenye maji ya chumvi), hasa katika maeneo yenye kina kifupi kama vile ghuba, viunga vya miambaza, au pembezoni mwa pwani.

Tofauti na magugu maji mengine ya baharini kama vile mwani (ambao ni aina ya alga), nyasi bahari ni mimea halisi inayofanana na nyasi ya kawaida ya nchi kavu—ina mizizi, shina, majani, na hata maua.

Mara nyingi hujulikana kama aina ya misitu ya buluu, nyasi za bahari, kama vile zile za nchi kavu, husaidia kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

Nyasi za baharini pia hufanya kama safu ya kwanza ya ulinzi kwenye ukanda wa pwani kwa kupunguza nishati ya mawimbi, kuwalinda watu kutokana na hatari inayoongezeka ya mafuriko na dhoruba.

Akitoa mada kuhusu uhifadhi na uhimilivu wa mifumo ikolojia ya baharini Mhadhiri Mwandamizi na Mkuu wa Shule ya Sayansi za baharini na Teknoojia ya Uvuvi kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Blandina Lugendo anasema kuwa sifa kuu za nyasi bahari humea chini ya maji ya chumvi kabisa amazo zina sifa nyingi kama ina mizizi inayoshikilia mchanga wa baharini, hivyo kusaidia kuzuia mmomonyoko wa fukwe.

Pia inazalisha oksijeni chini ya maji kupitia mchakato wa usanisinuru (photosynthesis).
Hutoa makazi na chakula kwa viumbe mbalimbali, kama kasa wa baharini, samaki.Ni muhimu kwa uchumi wa buluu, hasa kwa kusaidia mazingira ya wavuvi wadogo na utalii wa bahari.
Faida za nyasi bahari:

Nyasi bahari pia anasema kuwa zinasaidia kulinda fukwe dhidi ya mmomonyoko wa ardhi, kuvutia viumbe wa baharini na kuongeza samaki.Kuchuja maji ya bahari kwa kunyonya virutubisho na taka,kuhifadhi kaboni kutoka angani, hivyo kusaidia kupambana na mabadiliko ya tabianchi.

Mimea hii hupatikana kwa wingi katika mwambao wa bahari, hasa kwenye maeneo yenye utulivu kama vile mabwawa ya matumbawe, ghuba na mikoko.

Katika muktadha wa mabadiliko ya tabianchi na uharibifu wa mazingira ya bahari, nyasi bahari zimeendelea kutambuliwa kama nyenzo muhimu katika kulinda ikolojia ya bahari na maisha ya binadamu. Makala hii inachambua kwa kina umuhimu wa nyasi bahari, faida zake kwa mazingira na binadamu, pamoja na madhara yanayotokea pale zinapopotea au kuharibiwa.

Tofauti na majani mengine ya baharini kama vile mwani, nyasi bahari ni mimea kamili yenye mizizi, mashina, majani, maua na hata mbegu.

Dk Lugendo anasema kuwa nyasi bahari zina nafasi ya kipekee katika mfumo wa ikolojia ya baharini, na umuhimu wake unaweza kuonekana katika maeneo kama mazingira ya kuzaliana na makazi ya viumbe
ambao pia hutoa makazi kwa viumbe wengi wa baharini kama vile kaa, kamba, samaki wachanga,konokono, na viumbe vidogo vya plankton.

Mazingira haya yanasaidia viumbe hawa kuzaliana na kujificha dhidi ya wanyama wanaowawinda kwa kuimarisha afya ya bahari, Nyasi bahari huchangia kusafisha maji ya bahari kwa kufyonza virutubisho na uchafu, hivyo kusaidia kuweka maji katika hali safi na yenye oksijeni ya kutosha kwa viumbe wengine iki ni pamoja na kuzuia mmomonyoko wa fukwe.

Mtafiti Mwandamizi kutoka Asasi ya Utafiti Uvuvi Tanzania (TAFIRI) Dkt. Rushingisha George anasema wakiwa wanafanya tafiti wanatarajia matokeo ambayo yatatumika kuboresha shughuli zote za uhifadhi.

“Ili kupata matokeo chanya tumeona ni vyema kuwashirikisha wanahabari ili kufikisha taarifa hizi kwa wananchi kwa usahihi kwa sababu tafiti zetu zinatija kwa uhifadhi wa bahari,” anasema.

Anasema kwa sasa bahari inaathiriwa na ongezeko la asidibahari hivyo kuna mbinu za kukabiliana nazo kwa kupata taarifa sahihi, kufanya tafiti kuangalia athari za tatizo, kutoa elimu na kutekeleza mikakati inayoweza kupunguza athari kwa jamii.

Wadau wa Maendeleo ya Mali Bahari na Uchumi wa buluu wakiwa katika picha ya pamoja, katika kijiji cha Moa, wilayani Pangani, mkoani Tanga.