Na Salma Lusangi, JamhuriMedia, Unguja
Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Abeida Rashid Abdallah amesema Mpango Jumuishi wa Malezi Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto wa Miaka Mitano (5) utakapokamilika utakuwa nyenzo muhimu ya utekelezaji wa Sera ya Maendeleo ya Watoto na Malengo ya Kitaifa na Kimataifa.
Kauli hiyo ameitoa wakati akifungua kikao kazi cha siku tatu 01-3/09/2025 cha kuandaa Mpango huo kilichofanyaka katika Hotel ya Visitors Inn, Jambiani, Mjini Unguja kilicho andaliwa na Taasisi ya Afisi ya Rais Ufuatiliaji wa Utendaji Serikalini Zanzibar (ZPDB).
Amesema Mpango Jumuishi wa Malezi Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto wa Miaka Mitano unahimiza huduma za afya, chanjo, lishe bora na ulinzi wa mtoto na malezi yenye mwitikio, hivyo kuchangia moja kwa moja kwenye Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs),hususan lengo nambari nne (4) linalohusiana na Kupunguza Vifo vya Watoto chini ya Umri wa miaka mitano.

Amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia Ilani ya Chama cha Mapinduzi na mikakati yake ya maendeleo, imeweka kipaumbele kikubwa katika masuala ya Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto (ECD) ili kuhakilisha kila mtoto wa Kizanzibari anapata malezi bora ili aweze kufikia utimilifu wake (potential).
“Programu hii ni muhimu sana kwa kuwa unajikita katika kuhakikisha kila mtoto wa Kizanzibari anapata malezi bora, afya njema, lishe inayostahiki, ulinzi, na fursa ya kujifunza katika hatua za awali za maisha yake” Amesema Abeida.

Naye Naibu Katibu Mkuu Taaluma,Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Dkt Mwanakhamis Adam Ameir amesema Zanzibar kuna baadhi ya watoto wa darasa la tatu (3) mpaka la saba (7) hawajui kuandika kutokana na kukosa fursa ya kuijifunza katika umri wa awali.
Hivyo Wizara hiyo pia inafanya jitihada ya kuwafundisha walimu kuhusu Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya mtoto hasa katika ulaji kwani baadhi ya vyakula vinavyouzwa katika mashuleni sio salama ikiwemo malai na n.k.
Ameeleza kwamba elimu kuhusu Malezi Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto imeanzishwa katika Chuo cha Ualimu Nkutuma, wanafunzi wa kidato cha nne na sita waliopata divisheni ya kwanza na ya pili (one and two) wanafundishwa Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto ili waweze kuwalea Watoto katika misingi inayohitajika.
Kwa upande wa Wizara ya Afya, Akizungumza Naibu Mkurugenzi kinga Dkt Fatma Kabole amesema changamoto ya Afya ya akili kwa akinamama inaongezeka lakini Jitihada za Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Hussein Ali Mwinyi zimesaidia kuboresha huduma za Afya kwa kujenga hosipitali na kuimarisha vituo vya Afya kwa Unguja na Pemba.

Dkt Fatma amesema Wizara ya Afya imejenga hospital nne (4) katika ngazi ya Mkoa, vituo vya Afya 92 vimeimarishwa, vituo 52 ya Afya vituo vinatoa huduma za upasuaji huku vituo 11 vya akinamama vimeimarishwa ili kuwaondolea changamoto inayowakabili.
Akizungumza katika kikao kazi hicho, Mtalaam wa Hifadhi ya Mtoto kutoka UNICEF ndugu Ahmed Rashid Ali amesema kuna umuhimu mkubwa wa kuekeza katika Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto kwani faida yake ni sawa na kuwekeza shilingi moja katika biashara na kupata faida ya shilingi saba.
Amesema utafiti umeonesha asilimia 18 watoto wameduma huku asilimia 40 hawakufikia viwango vya Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali, hivyo Shirika la UNICEF linafanyakazi ya kushirikina na Serikali ya Mapinzudi Zanzibar kupata kinga na matibabu ya changamoto iliyopo.
Mapema akizungumza, Mratibu wa Programu ya Malezi, Makuzi na maendeleo ya Awali ya Mtoto kutoka ZPDB) Dkt. Maryam Issa amesema lengo la Programu hiyo ni kuhakikisha watoto 276,000 wa Zanzibar wanakua katika mwelekeo unaofaa kwa kuhakikisha wanapata huduma za afya, lishe, ulinzi na usalama wa mtoto ifikapo 2030.

Amesema shughuli mbali mbali zimekuwa zikitekelezwa kupitia program hiyo ikiwemo kufanya utafiti wa hali ya malezi na makuzi ya awali ya mtoto ya Zanzibar (ECD base line survey), ambapo miongoni mwa matokeo ya utafiti huo yameonesha kwamba Takribani asilimia 32 ya watoto wenye umri wa miaka 0–3 Zanzibar wamechelewa kimaendeleo.
Pia Dkt Maryam amesema Programu hiyo imefanya utafiti mdogo wa kuangalia huduma rafiki za Malezi na makuzi ya mtoto katika masoko, hospitali na skuli za maandaalizi kwa Unguja na Pemba. hali ambayo inaonesha kuwa huduma hizo hazipo, hivyo programu inakwenda kuweka huduma hizo katika maeneo niliyoyataja.
Aidha amesema Maandalizi ya Mtaala wa Malezi na Makuzi ya Awali ya Mtoto kwa wahudumu wa afya ngazi ya jamii yamekamilika. Na sasa tayari mafunzo kwa wahudumu hao wa afya yameanza katika maeneo ya Unguja na hatua inayofata wanatarajia Kwenda kisiwani Pemba kutekeleza.

Naye Afisa Muandamizi kutoka Wizara ya Kilimo, Umwagiliaji Maliasili na Mifugo amesema Wizara hiyo inazalisha asilimia 60 ya vyakula vya mboga mboga, protini, vitamini lakini shida iliyopo ni katika uelewa wa mlaji kwani tatizo lipo kwa wenye watu wenye uwezo na wasiokuwa na uwezo hivyo elimu ya lishe inahitajika kwa jamii.
Programu ya ECD inaratibiwa na Afisi ya Rais Ufuatiliaji na Usimamizi wa Utendaji Serikalini (ZPDB) na inatekelezwa kwa mashirikiano kati ya Wizara ya Afya, Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali, Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto na Wizara ya Kilimo Umwagiliaji,Maliasili na Mifugo.


