Na Zulfa Mfinanga, JamhuriMedia, Arusha

Paul Christian Makonda ameibuka mshindi wa nafasi ya Ubunge wa Jimbo la Arusha Mjini kwa kupata kura 9,056 ambazo ni sawa na asilimia 97.63 ya kura zote halali.

Ushindi huu unamuweka mbele kwa kiasi kikubwa dhidi ya wagombea wengine sita waliokuwa wakiwania nafasi hiyo katika uchaguzi wa ndani ya Chama cha Mapinduzi (CCM).

Akitangaza matokeo hayo, Mkurugenzi wa Uchaguzi ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Arusha Timothy Sanga alisema jumla ya wajumbe 10,186 walipaswa kupiga kura, lakini waliopiga kura ni 9,276 sawa na asilimia 91.01, kura halali zilikuwa 9,265 huku kura 11 zikiharibika.

Washindani wa Makonda walijikuta wakipata kura chache, Mustapha Said Nassoro alipata kura 83 (0.89%), Hussein Omarhajji Gonga kura 46 (0.50%), Ally Said Babu kura 28 (0.30%), Aminatha Salash Toure kura 26 (0.28%), Lwembo Mkwavi Mghweno kura 16 (0.17%), na Jasper Augustino Kishumbua kura 10 (0.11%).

Matokeo haya yanaonyesha uungwaji mkono mkubwa kwa Makonda kutoka kwa wajumbe wa CCM Arusha Mjini na ni ishara kuwa ana nafasi nzuri ya kupeperusha bendera ya chama hicho kuelekea uchaguzi mkuu iwapo atapitishwa rasmi.

Uchaguzi huu wa ndani ni hatua muhimu katika mchakato wa kupatikana kwa wagombea wa nafasi mbalimbali ndani ya chama hicho tawala.