Marais wa zamani wa Marekani Barack Obama na Bill Clinton, wametoa wito kwa Wamarekani kusimama na kutetea maadili ya nchi yao baada ya mauaji ya pili ya raia mjini Minneapolis.

Marais wa zamani wa Marekani Barack Obama na Bill Clinton, wametoa wito kwa Wamarekani kusimama na kutetea maadili ya nchi yao baada ya mauaji ya pili ya raia mjini Minneapolis yaliyofanywa na maafisa wa uhamiaji, mauaji ambayo Donald Trump amesema ni matokeo ya vurugu za chama cha Democratic.

Serikali ya Trump imekuwa ikikabiliwa na shinikizo linaloongezeka kuhusu msako wake mkali dhidi ya wahamiaji, hasa baada ya maafisa wa shirikisho kumpiga risasi na kumuua Alex Pretti, muuguzi wa chumba cha wagonjwa mahututi mwenye umri wa miaka 37, siku ya Jumamosi, wakati wakijibizana naye kwenye barabara yenye barafu.

Tukio hilo lilitokea chini ya wiki tatu baada ya afisa wa uhamiaji kumpiga risasi na kumuua Renee Good, naye akiwa na miaka 37, ndani ya gari lake katika mji huo huo wa Kati-Magharibi.

Maafisa wa utawala wa Trump walidai haraka kuwa Pretti alikusudia kuwadhuru maafisa—kama walivyodai pia kuhusu kifo cha Good—wakitaja kuwa alijihami kwa bastola.

Hata hivyo, video iliyosambaa sana kwenye mitandao ya kijamii na kuthibitishwa na vyombo vya habari vya Marekani ilionyesha kuwa Pretti hakutoa silaha yoyote, na maafisa walimpiga risasi sekunde chache baada ya kumwagia usoni kemikali inayowasha na kumtupa chini.