Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Pwani
Ofisi ya Msajili wa Hazina (OMH) imejiwekea lengo la kukusanya kiasi cha Sh 2 trilioni kama mapato yasiyo yakikodi katika mwaka wa fedha 2025/26, imebainishwa.
Hayo yalisemwa Jumatatu, Julai 28, 2025, na Msajili wa Hazina Bw. Nehemiah Mchechu wakati wa ufunguzi wa mafunzo elekezi ya siku nne kwa wakuu wa taasisi za umma yaliyoandaliwa na OMH kwa kushirikiana na Taasisi ya Uongozi.

Kiasi kinachotarajiwa kukusanywa ni zaidi ya lengo la Sh1.6 trilioni ambalo serikali iliiwekea Ofisi ya Msajili wa Hazina kukusanya mwaka huu wa fedha.
“Ili tuweze kufikia lengo letu la kukusanya Sh2 trilioni itatubidi tuongeze bidii kwa asilimia 100 ya tulivyokuwa tunafanya mwaka wa fedha uliopita,” alisema Bw. Mchechu.
Katika mwaka wa fedha uliopita (2024/25) Ofisi ya Msajili wa Hazina ilikusanya kiasi cha Sh1.028 trilioni kama mapato yasiyo yakikodi.
Miongoni mwa vyanzo vikuu vya mapato yasiyo yakikodi ni Gawio—Mapato haya yanatokana na Mashirika na Taasisi zinazofanya biashara na yanakusanywa kwa mujibu wa Sheria ya Makampuni SURA 212 (Kifungu cha 180) na Sheria ya Mashirika ya Umma Sura 257 (Kifungu cha 15(2)(b)).

Vyanzo vingine ni michango ya asilimia 15 ya mapato ghafi— Kifungu cha 12 (3) cha Sheria ya Fedha za Umma Sura 348 kinazitaka taasisi za umma (zisizo kwenye kundi la gawio) kuwasilisha asilimia kumi na tano ya mapato ghafi kwenda Mfuko Mkuu wa Serikali.
Pia kuna mapato mengineyo ambayo huhusisha asilimia 70 ya mapato ya ziada ya taasisi za umma, marejesho ya mikopo na riba na mawasilisho yatokanayo na mtambo wa kuhakiki na kuwezesha mawasiliano (TTMS) kati ya Tanzania na nchi nyingine.
Msajili wa Hazina anaamini kuwa mafunzo elekezi kwa Kundi hili la pili linalojumuisha watendaji wakuu 114 wakiwemo walioteuliwa hivi karibuni pamoja na walioko katika nafasi zao kwa muda mrefu lakini hawakubahatika kupatiwa mafunzo, yatakuwa chichu ya mageuzi katika mashirika ya umma.
Lengo la mafunzo haya ni kuwaimarisha wakuu wa taasisi katika nyanja za uongozi na maadili, uwajibikaji wa kifedha na usimamizi wa uwekezaji wa umma ambao hadi kufikia mwaka 2023/24 umefikia takribani Sh86.25 trilioni, ambapo kiasi hiki kimewekezwa katika taasisi za umma 252 na kampuni ambazo Serikali ina hisa chache 56.