Meneja wa kampeni za Mgombea Urais wa ACT Wazalendo, Ismail Jussa Ladhu, amewataka Wazanzibari kujitokeza kwa wingi ifikapo Oktoba 29 ili kumchagua Othman Masoud Othman, akisema huu ndio wakati wa kurejesha heshima, utu na thamani ya wananchi wa Zanzibar.

Akizungumza katika uzinduzi wa kamati za ushindi, Jussa alieleza kuwa moja ya dhulma kubwa chini ya utawala wa sasa ni kunyimwa nafasi Wazawa katika sekta ya afya.

Alifafanua kuwa madaktari bingwa wazawa wa Zanzibar wanalipwa mishahara duni ya milioni moja pekee, huku madaktari waliotoka nje wakilipwa hadi milioni saba.

“Wazanzibari wamegeuzwa na kuonekana kama watu wasiojitambua, kana kwamba wao hawawezi. Hii ni dharau kubwa.

Wazanzibari ni watu weledi, watu wa maarifa, wenye uwezo kwa karne na karne. Sasa ndio wakati wa kurejesha hadhi yao kupitia ACT Wazalendo na mgombea wetu, Othman Masoud,” alisema Jussa kwa msisitizo.

Aidha, Jussa aliwataka wanachama wa chama hicho kutowabagua wanachama wa CCM, akieleza kuwa baadhi yao hawajui wanachokifanya, na wengi wao wamechoshwa na hali ya sasa. “Wananchi wanahitaji mabadiliko, na hawataki tena kuendelea kufanywa wajinga katika nchi yao wenyewe,” aliongeza.

Meneja huyo wa kampeni alifichua pia kuwa Chama cha Mapinduzi (CCM) kimekuwa kikifanya mchango mchafu, ukiwemo kuwafuata wagombea wa ACT na kuwapa mafurushi ya fedha ili wajiondoe kwenye kinyang’anyiro.

“Lakini wanarudi na fedha zao mikononi, kwa sababu Wazanzibari wanajua wanachokitaka, na hawatauzwa tena,” alisema.

Jussa alionya pia kuhusu mikakati ya ndani ya CCM kujaribu kuwarubuni mawakala wa ACT Wazalendo katika uchaguzi huo, akisema huo ni upuuzi mtupu kwa sababu wananchi wamechoshwa na sasa wanataka mabadiliko ya kweli.

Kwa shauku kubwa alihitimisha hotuba yake akisema: “Huu ndio wakati wa Zanzibar mpya. Huu ndio wakati wa kuandika historia. Huu ndio wakati wa kumchagua Othman Masoud,kiongozi mwenye hekima, uadilifu na dhamira ya kuwatumikia wananchi.

“Oktoba 29 si siku ya kawaida, ni siku ya ukombozi wa Zanzibar.”