Mwenyekiti wa Taifa wa ACT-Wazalendo Mheshimiwa Othman Masoud Othman, amesema ni wajibu kwa viongozi wa dini kuangalia haki, utulivu na amani ya kweli, wanayoihitaji Wananchi wote, kwaajili ya Maendeleo ya Taifa zima.

Amesema, viongozi hao ndio wenye dhima ya kuhakikisha haki inatendeka, na ambayo ndiyo msingi mkubwa wa maendeleo ya Nchi, kwani Sauti yao inafika mbali zaidi.

Mheshimiwa Othman, ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, ameyasema hayo Agosti 28, 2025, alipokutana na kubadilishana mawazo na Askofu wa Jimbo la Catholic Zanzibar, Mhasham Augustine Shao.

Maongezi hayo, ambayo yamehusisha pia kukabidhi Ripoti Maalum ya Hali ya Kisiasa Nchini na Nafasi ya chama hicho katika kutafuta amani ya kudumu kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba mwaka huu, yamefanyika huko Ofisi za Kanisa la ‘Roman Catholic’ la St. Joseph, Minara Miwili, Shangani Mjini Unguja.

Amefahamisha kuwa viongozi wa kidini na kanisa hilo ambao ni alama ya hekima, umoja, utengamano na amani ya kweli, hasa hapa visiwani, wanayo sauti ya kuzungumza wakasikika mbele ya watawala, hata wale ambao si wasikivu wa vilio vya Watu.

Ameeleza kwamba, hilo kwa sasa ni katika hitajio la lazima kwani yapo mambo mengi yameshajiri ambayo hayaoneshi mwelekeo mwema nchini, kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba Mwaka huu.

“Sisi ACT-Wazalendo tumefanya juhudi mbali mbali za kutafuta Amani ya Kudumu hapa Visiwani, na katika Tanzania yote, ikiwemo hata kukubali kuendelea na Serikali ya Umoja wa Kitaifa, licha ya kutoka katika uchaguzi ulioacha maumivu na makovu makubwa kwa Maelfu ya Wanachama wetu na Wananchi wote”, amesema.

Amebainisha kuwa, moja ya Madhumuni ya Serikali ya Umoja wa Kitaifa, ni kuiweka Nchi katika mstari wa maridhiano na mashirikiano; hali inayopelekea kuondoa misigano isiyo ya lazima ya kisiasa, ndani ya Jamii ya Wazanzibari, wenyewe kwa wenyewe.

Akieleza baadhi ya mambo ambayo walikubaliana na Watawala waliopo sasa Madarakani, ambao amesema wako kimya kama kwamba hakujatokea chochote hapo awali, Mheshimiwa Othman ameanisha kuwa ni pamoja na Kutokuwepo kwa Kura ya Mapema; Kuundwa Tume Huru ya Uchunguzi wa Mauwaji dhidi ya Wananchi katika Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2020; Kupatiwa Vitambulisho vya Mzanzibari kwa ambao Wamenyimwa Haki yao hiyo ya Kisheria; na Kujengewa Imani Wananchi juu ya Kuwepo Uchaguzi wa Huru na Haki, kwa Kuondoshwa katika Usimamizi, wale Waliohusika na Wakasababisha Maafa hayo.

Aidha, amesema Dhamira ya Chama hicho siyo kupata Vyeo, bali ni Amani ya Kweli na ya Kudumu, kwaajili ya mustakbali mwema wa maendeleo Nchi, na itakayoiweka katika utulivu wa kuendelea.

“Viongozi wa Chama chetu kwa pamoja tuliwahi kukutana na Rais wa Zanzibar na tukamuahidi kwamba tutampa mashirikiano ya kutosha, bali ahakikishe matakwa ya wananchi, yakiwemo kurudisha imani na kusimamia upatikanaji wa haki zao, jambo ambalo kama kwamba amelipuuzia, na hakuna kinachofanyika juu ya hilo”, amefafanua Mheshimiwa Othman.

Hata hivyo, Mheshimiwa Othman amesisitiza kwa kusema, “haijalishi nani atapata nafasi gani baada ya uchaguzi, yote ni matokeo na matakwa ya wananchi, bali la muhimu kwetu sisi kuona haki inatendeka, na maamuzi ya Wananchi yanaheshimiwa, katika kuchagua Viongozi wanakubaliana nao, bila ya shinikizo wala matokeo ya kupangwa”.

Kwa upande wake, Makamu Mwenyekiti wa ACT-Wazalendo Zanzibar, Zanzibar Ismail Jussa, amesema siku zote iwapo Taifa likisimama katika Misingi ya Haki, Amani na maendeleo yatapatikana.

“Si vyema kwa Kamati ya Amani kutumika mwishoni baada ya mambo kuchafuka, na badala yake wasimamie sasa kwa kuyapazia sauti, na kuyasema kwa uwazi yale mabaya ambayo yanaweza kuwa vichocheo vya kuvunjika kwa amani nchini”, ameongeza kiongozi huyo.

Naye, Baba Askofu Mhashamu Augustino Shao, amefahamisha kuwa mbegu ya Amani ya Kweli, ni pale kila mtu kupata haki yake, na wala si vinginevyo.

“Serikali ya Umoja wa Kitaifa imekuwa ndiyo mlango wa amani na utulivu, na ni kichocheo kikubwa cha uchumi wa hapa Zanzibar kupitia utalii; hivyo lazima heshima ya Haki na amani ipatikane kwani bila ya hayo, kinachobaki ni uoga uliofichika”, ameeleza Baba Askofu.

Mazungumzo hayo ni Muendelezo wa ACT-Wazalendo kuwakabili viongozi wa dini, kwa Dhamira ya Kuwaelezea hali Halisi ya Kisiasa, na Nafasi ya Chama hicho katika kutafuta amani ya kudumu nchini.

Katika Msafara wake, Othman ambaye ni mgombea wa Nafasi ya Urais wa Zanzibar kupitia ACT-Wazalendo, ameambatana na viongozi mbali mbali Waandamizi wa Chama hicho.