Na Andrew Chale, JamhuriMedia, Shinyanga
TAASISI ya Pamoja Tutashinda Tanzania (PATUTA) imeshiriki katika tukio kubwa la kusimikwa kwa Mtemi mpya wa 24 wa Busiya Austin Makani Makwaia ‘Chief Makwaia wa III’ katika Ikulu ya Busiya Ukenyenge Wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga, Juni 28, 2025.
Zaidi ya wanachama na viongozi 25 wa PATUTA wamejumuika pamoja na jamii ya wana Busiya katika sherehe za kimila zilizojumuisha shamrashamra za vikundi vya ngoma za asili na masuala ya matambiko ya Kichifu ya Jamii hiyo ya Wasukuma.

Katika tukio hilo, Mkurugenzi wa PATUTA, Dk Aiden Ndaombwa ameshukuru kwa niaba ya wanachama wa taasisi hiyo kwa namna ya kipekee ya ushirikiano wao na Jamii ya Machifu kwani wanaamini katika kuendeleza Mila na tamaduni za mtanzania kupitia Machifu wa sehemu zote ndani na nje ya Nchi.
“Tumefika Shinyanga katika kumuunga mkono Mwanachama mwenzetu wa PATUTA
Chifu Makwaia III ambaye ameapishwa rasmi.
Dhima ya Taasisi yetu pia kuunga mkono juhudi za kuendeleza jamaii za Machifu, lakini pia kama ilivyo, Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan ni Chifu Hangaya na ameleta taswira ya kuendeleza Uchifu nchini.

PATUTA tunaungana nae kwa mikono miwili na tunaendelea kushirikiana nae, Lakini pia katika kuona tunasonga mbele na kushinda kwa pamoja” Amesema Dr Aiden Ndaombwa.
Katika tukio hilo, Chief Makwaia III amesimikwa nafasi hiyo baada ya aliyetoka Edward Makwaia ‘Chief wa Pili” wa 23 ambaye amestaafu kwa hiyari.
Awali akizungumza baada ya kukabidhi Uchifu huo, Chief Edward amesema amekaa madarakani toka mwaka 2009 na ameamua kustaafu ili kumuachia Chief Makwaia III.
Aidha, baada ya sherehe hizo ya kusimikwa Chief Makwaia wa III’, kwa sasa anaanza rasmi mara moja shughuli za Kichifu yeye na Ngore wake (Mkewe) ambapo kwa pamoja walikabidhiwa Vifaa mbali mbali vya kimila na Baraza la Jadi la Jamii ya Wana Busiya.

Miongoni mwa majumu ikiwemo tukio la tamasha kubwa la Sanjo ya Busiya au likijulikana kama: 77Fest ambalo hufanyika Kila mwaka kuanzia tar 05/07 na kilele chake ni 07/07 na tamasha hili ni maalumu Kwa maonyesho ya utamaduni, Ngoma za asili na michezo ya asili.
Awali tukio hilo la kusimikwa Chief Makwaia wa III, Mtemi ameweza kuwasha moto wa mwaka mzima, huku pia akiziombea mbegu kwa ajili ya wakulima na tamasha hilo la Sanjo ya Busiya.






