KIONGOZI Mkuu wa Kanisa Katoliki Duniani Papa Leo XIV ametangaza Jumamosi sera za uongozi wake, huku akiitaja teknolojia ya akili mnemba kama moja ya changamoto kubwa kwa ulimwengu.

Papa Leo alisema teknolojia hiyo ya akili mnemba (AI) inahatarisha harakati za kutetea ubinaadamu, haki na ajira.

Kwenye hadhara yake ya kwanza tangu alipochaguliwa siku ya Alhamisi, Papa leo amesema yuko tayari kuendeleza mageuzi yaliyoidhinishwa na Azimio la Pili la Baraza la Kanisa miaka ya 1960 ambayo yamesaidia kupatikana kwa ustawi mpya wa Kanisa hilo lenye waumini bilioni 1.4.

Papa Leo XIV ameweka wazi kwamba atafuata sera za mageuzi za mtangulizi wake Papa Francis na kulifanya Kanisa Katoliki kuwa sehemu inayohubiri umoja, kuwasikiliza waamini wote hasa wale wasiojiweza na waliotengwa.

Wakatoliki wa Nigeria na DRC wampongeza Papa Leo XIV
Wakati Kiongozi mpya wa kanisa Katoliki duniani, Papa Leo XIV akiongoza siku ya Ijumaa misa yake ya kwanza, watu katika mataifa mawili ya Afrika yenye waumini wengi wa Kikatoliki ya Nigeria na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, walidhihirisha furaha yao huku wakitumai kuwa Papa huyo ataendeleza misimamo ya kiliberali ya mtangulizi wake.

Wakaazi wa mji mkuu wa Kongo, walifurahishwa na kuchaguliwa kwa Papa Leo XIV licha ya kwamba walikuwa na matumaini ya kumuona askofu mkuu wa jiji la Kinshasa Kadinali Fridolin Ambongo anakuwa papa wa kwanza mweusi. Ifahamike kuwa karibu asilimia 40 ya raia milioni 100 wa Kongo ni wakatoliki.

Rais wa Nigeria Bola Tinubu alisema kuchaguliwa kwa Papa Leo XIV kunafungua ukurasa mpya katika historia ya Kanisa Katoliki chini ya misingi ya upendo na ubinadamu hasa kwa wale wasiojiweza.