Na Magrethy Katengu,Jamhuri Media , Dar es Salaam.

Waandishi wa habari na mabloga wametakiwa kuelimisha jamii kuhusu sheria ya ulinzi wa taarifa binafsi, ili kuzuia uvunjifu wa faragha na kuepusha madhara ya kisheria.

Wito huo umetolewa Dar es Salaam Agosti 11,2025 na Mkuu wa Uhusiano na Mawasiliano kwa Umma wa Tume ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi (PDPC), Innocent Mungy, wakati wa mafunzo maalum kuelekea Uchaguzi Mkuu, yaliyoandaliwa na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kwa ombi la Mtandao wa Mabloga Tanzania (TBN). ambapo amesema mabloga wana nafasi kubwa ya kuelimisha umma kuhusu sheria hiyo, hasa katika kipindi cha uchaguzi, na kuwaonya kuepuka kuchapisha taarifa binafsi za watu au wagombea.

“Ni kosa kisheria kuingilia faragha binafsi ya watu,atakayebainika akishtakiwa adhabu yake ni kali. Bloga mna wajibu wa kulinda faragha na kuepuka taarifa zinazoweza kuvunja sheria,” amesema Mungy.

Sambamba na hayo Mungy amesema kuwa maendeleo ya teknolojia yameongeza fursa na changamoto katika uandishi, hivyo mabloga wanapaswa kutumia majukwaa yao kwa uwajibikaji mkubwa. Pia aliahidi kuchangia mabloga ili waweze kusajili majukwaa yao kama inavyotakiwa kisheria.

Naye Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dkt. Egbert Mkoko, amewakumbusha washiriki kufuata miongozo rasmi ya uandishi wa habari za uchaguzi, akisisitiza umuhimu wa blogu katika kutoa taarifa sahihi kwa jamii.

Kwa upande wake, Afisa wa Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari, Rehema Mpagama, meeleza kuwa waandishi watakaoruhusiwa kuripoti uchaguzi ni wale tu wenye ithibati, kwa mujibu wa sheria.

Aidha Mwenyekiti wa TBN, Beda Msimbe, ameishukuru Serikali chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fursa ya mafunzo hayo kupitia TCRA, akisema yatasaidia kuongeza weledi na kuimarisha usalama wa taarifa wakati wa uchaguzi.