Na Kulwa Karedia, JamhuriMedia, Sumbawanga

Mratibu wa Kampeni Kanda za urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM),Kanda ya Magharibi na Waziri Mkuu mstaafu, Mizengo Pinda amewafunda na kuwataka wagombea ubunge wa Mkoa wa Rukwa kuacha tofauti zao walizonazo.


Pinda ametoa kauli hiyo alipopewa nafasi ya kusalimia maelfu ya wananchi wa mkoa huo wakati wa mkutano wa kampeni za mgombea urais wa chama hicho Samia Suluhu Hassan mjini Sumbawanga leo Oktoba 19,2025.


“Wakati wa mchakato wa kura za maoni kulikuwa na mambo fulani fulani, tunatamani maendeleo na umoja kwenye mkoa wetu.
“Kutokana na hali hii nawaomba wabunge wetu wateule tutafute kila namna hii iwe timu moja na yenye mawazo ya pamoja kwa ajili ya maendeleo ya wananchi wetu.


“Tunatakiwa kuwa na mawazo ya kwenda mbele zaidi, kila mmoja wetu jengeni umoja mkubwa, kaeni pamoja tutoke hapo tulipo.
“Kila mbunge awe mwalimu kwa madiwani kaeni mlete maendeleo, yaliyopita si ndwere tugange yajayo,”amesema.


Amesema mgombea urais wa CCM, Rais Samia ni kiongozi makini na mwenye nia njema kwa Watanzania.


“Hata alipokwenda bungani kule kuandaa filamu ya Royol Tour imesaidia mno kuleta watalii ambao sasa wamefika milioni 5.
Pinda amemuomba Rais Samia kusaidia changamoto zilizopo katika Bandari ya Kasanga ili iweze kufanya kazi vizuri.


“Nilibata bahati ya kutembelea Bandari ya Kasanga nilikuta ina hali mbaya, niliuliza maswali mengi mno, lakini sikupata majibu ya kuridhisha.


“Naomba ututupie macho pale bandarini tuwe kama wenzetu wa Kalema ambao mambo yao yako vizuri, tunaomba tupate barabara ya lami ambayo itasaidia magari kwenda pale kupeleka na kuchukua mizigo kutopata changamoto ndogo ndogo,”amesema.


Amesema kuimarika kwa bandari hiyo kutasaidia kukuza uchumi wa mkoa na nchi za jirani kama Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC),Zambia na Rwanda.


Kuhusu maendeleo ya mkoa huo, Pinda amesema umepiga hatua kubwa tofauti na miaka ya nyuma.


“Tumekuwa na maendeleo tofauti na miaka ya nyuma, tumekuwa na barabara nzuri za kiwango cha lami, kutoka Dar es Salama hadi Sumbawanga kilomita 1,800 hivi lakini sasa mambo mazuri,”amesema.


Amesema mkoa huo ulikuwa nyuma katika sekta za elimu na uchumi, lakini juhudi kubwa zilizofanywa na serikali zimebadili taswira ya nyuma
Amewashauri wana Rukwa kupeleka watoto shule wasome hasa masomo ya sayansi ambapo wamejenngewa shule maalumu.
Mkoa wa Rukwa unashika namba mbili katika uzalishaji wa chakula ukitanguliwa na Ruvuma.