Na Aziza Nangwa, JamhuriMedia, Dar es Salaam

Mkurugenzi mtendaji wa Kampuni ya Usafirishaji ya PMM, Dk Judith Mhina Spendi, amesema kuwa kuwasili kwa wageni kutoka Oman kwenda kwenye ofisi yao ya ni fursa ya kukuza uchumi wao na taifa kwa ujumla.

Dk Judith ameyasema hayo mara baada ya kupokea ugeni kutoka nchini Oman kwa ajili ya kuangalia fursa mbalimbali za uwekezaji zinazofanywa na kampuni ya usafirishaji mizigo ya PPM ambapo katika msafara huo waliambana na Mheshimiwa Balozi na mkurugenzi wa idara ya Mashariki ya Kati Abdallah Abasi Kilima

Amesema amefurahishwa sana na ujumbe huo kutoka Oman kwani utasaidia kukuza biashara yao na Oman, kwa sababu wataweza kupata fursa ya kusafirisha bidhaa zinazopatikana hapa Tanzania, hasa mazao ya mifugo na kilimo kama vile mbuzi, ng’ombe, chumvi, mboga za majani, na maua kwenda Oman na zinazokuja Tanzania.

‘’Sisi kama wasafirishaji tunaona hii ni fursa kubwa kwetu na serikali kwa ujumla, kwani itasaidia kukuza uchumi wa taifa kwa sababu tuna uwezo wa kusafirisha bidhaa kwa njia zote tutakuwa tunawapeleka kontena nyingi kupitia meli zetu kwa kusafirisha mazao kutoka Tanzania’’amesema.

Aidha ameongeza kusema kuwa kupitia ushirika huo watatumia fursa hiyo kuleta bidhaa ya Salfa kutoka Oman kwani hapa nchini inahitajika hasa hasa katika matumizi ya migodi na bidhaa zingine kama mafuta, pamoja na vifaa vya ujenzi kuja Tanzania.

Dkt. Judith ameushukuru uongozi wa Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kufungua milango ya kuwaleta wawekezaji kuja nchini kukuza uchumi wetu kupitia uwekezaji katika sekta mbalimbali.

Pia , amewataka wawekezaji wengine kuja kujiunga na kampuni yao kwa sababu bado wana fursa nyingi za kuwekeza, ikiwemo kwenye kilimo, madini, na bandari kavu.

Baadhi ya wageni waliotembelea kampuni ya usafirishaji ya PMM

Balozi na mkurugenzi wa idara ya Mashariki ya Kati Abdallah Abasi Kilima amesema wamekuwa na ugeni huo wa wafanyabiashara kutoka Oman kwa takribani siku saba sasa wamekuwa wakitembelea maeneo mbalimbali.

Kilima amesema lengo la kuwatembeza katika kampuni ya PMM, ni kuwaonyesha uwezo wa kampuni ya hapa nyumbani katika suala zima la usafirishaji na fursa zingine walizokuwa nazo ili kuwahamasisha kufanya uwekezaji.

Amesema lengo la ujumbe huu ni kukuza biashara kati ya Oman na Tanzania, kwani huwezi kukuza biashara kama huna usafiri wa uhakika kama ilivyo kampuni ya PMM, ambayo ina uwezo wa meli tatu zitasaidia kuleta na kusafirisha mizigo nje na ndani ya nchi, ambazo ziko tayari kwa biashara ya kusafirisha kati ya Oman na Tanzania.

PMM itasaidia sana kusafirisha bidhaa mbalimbali kutoka Oman kuja Tanzania na kutoka Tanzania kwenda Oman,kwa hiyo, kampuni hii itakuwa kiunganishi cha biashara kwa kuunga mkono jitihada za serikali katika biashara kati ya Tanzania na Oman.

Lengo kuu ni kukuza biashara kati ya Omani na Tanzania. Kwa hiyo, nchi zote mbili, kutokana na kupatikana kwa usafiri wa uhakika kutoka Tanzania kwenda Omani kupitia PMM, biashara zitakuwa imara.

Mchumi kutoka katika msafara huo, Salim Albu Saidi, amesema wameshukuru sana kuja kutembelea Tanzania kuona fursa za uwekezaji katika maeneo mbalimbali.

‘’Hii itakuwa ni fursa kwa nchi zote mbili kufanya biashara au uwekezaji wa pamoja, kwani kuna bidhaa ambazo zinaweza kwenda Omani na bidhaa zitakazotoka Omani kuja Tanzania’’amesema.