Na Deodatus Balile, JamhuriMedia, Morogororo

Leo ni siku 10 tangu Oktoba 29, 2025 siku tuliyofanya Uchaguzi Mkuu wa Rais, wabunge na madiwani. Naandika makala hii baada ya kutoka kanisani.

Nimekaa, nimetafakari, nikawaza na kuwazua. Yamenijia maono nikaona kupitia makala hii, nizungumze na Watanzania wenzangu juu ya uchaguzi, vurugu zilizotokea baada ya uchaguzi na wapi tunapaswa kuelekea kama nchi.

Katika kulifanya hilo nimekumbuka mambo mawili; Yesu Kristu na mzee jirani yangu. Naomba nianze na haya mawili, ndipo nije kwenye andiko langu.

Biblia Takatifu katika Injili ya Luka 5:31-32 Yesu aliwajibu wanafunzi – mafarisayo na walimu wa sheria – walionung’unika kuwa amemwita mtoza ushuru Lawi amfuate, kisha Lawi akamwandalia karamu akala na watoza ushuru wengine, ambao wao waliowaona kuwa ni wadhambi.

Yesu alisema: “Wenye afya hawamuhitaji daktari; wanaomuhitaji ni wale walio wagonjwa. Sikuja kuwaita watu wema, bali wenye dhambi, wapate kutubu.”

Jambo la pili, nilikuwa na mzee jirani yangu kijijini kwetu Bukoba. Aliniambia: “Mwanangu, siku ukiwa na hasira, usifanye uamuzi, ukiwa na furaha, usitoe ahadi.”

Mambo haya mawili yataniongoza katika makala hii, lakini msingi mkuu utakuwa ni kuusema ukweli na ukweli utatuweka huru.

Nitahadharishe mapema. Inawezekana baadhi ya ukweli nitakaousema usiupende, ila nitaomba uutafakari na kuangalia kama una mantiki au la. Nipo tayari kukosolewa baada ya kuandika makala hii. Sitatumia lugha ngumu, bali nitatumia lugha ya kujenga matumaini.

Sitanii, nianze kwa kutoa pole kwa Watanzania wenzetu walipoteza maisha, waliojeruhiwa na hata waliopoteza mali zilizochomwa moto au kuporwa. Thamani ya maisha haipimiki kokote. Tulinde maisha ya Watanzania isitokee tena.


Ni ukweli ulio wazi kuwa siku ya kupiga kura na kesho yake, vijana waliingia barabarani kuandamana. Katika maandamano hayo, vituo vya mwendokasi, magari ya watu binafsi (hasa malori), vituo vya mafuta, ofisi za serikali na za Chama Cha Mapinduzi (CCM) vilichomwa moto.


Katika vurugu hizo, askari kadhaa waliokuwa wanalinda usalama wa raia, waliuawa pia. Zilipatikana taarifa za watu waliokuwa kwenye Noah wakipiga risasi watu hovyo.

Hawa walikuwa wamevaa sare za polisi. Taarifa zimepatiakana na Rais Samia amesema, lakini pia hata wananchi walioko mitaani wanasema hawa waliokuwa wanaua watu hovyo kwa kupiga risasi si Watanzania. Na kweli imethibitika hawakuwa Watanzania. Swali, ni nani aliwaleta hawa? Sina jibu.


Jambo moja nimelisikia, Polisi na Jeshi waliweka mtego wa mafuta kwa wauaji hawa waliokuwa kwenye Noah, walipokwenda kwenye kituo kimoja kujaza mafuta wakatiwa mbaroni Oktoba 30, 2025 na huo ndio ukawa mwanzo wa amani kurejea.

Wananchi wengi wamesema kuwa wauaji hawa walikuwa hawajui hata Kiswahili vizuri. Je, sababu za kuandamana ni zipi? Niruhusu nihamie sehemu ya pili ya makala hii, kisha nitazigusia ambazo nimezisoma kwenye mitandao ya kijamii na wanazoniambia wanaonipigia simu.


Sitanii, katika dunia tunayoishi, ni wazi tunashuhudia mambo mengi. Ni wazi yapo yanayotupendeza, lakini yapo tusiyoyapenda. Jambo moja, ni kutambua tuliposimama.

Niseme kwa mfano ulio na uhalisia, kwamba tupende tusipende katika huu mkwamo tuliomo, lazima atakuwapo Mtanzania mmoja wa kutuongoza kutoka hapa tulipokwama, na bila kupepesa macho, Mtanzania huyu si mwingine, ni Rais Samia Suluhu Hassan.

Narudia, hili inawezekana msomaji hutalipenda, lakini ni kanuni ya asili kuwa hakuna mgeni kutoka nje ya nchi anayeweza kusuluhisha tatizo la nchi nyingine yoyote, bila Rais aliyeko madarakani kuridhia au kushirikishwa na kuamua kushiriki.

Nikukumbushe tu, kuwa huwezi kumshawishi Rais yeyote aliyeko madarakani kushiriki mazungumzo kama hutambui ushindi wake. Yapo mazingira ambayo mazungumzo yanaweza kuendelea bila wahusika kutambuana, kama ilivyo mazungumzo ya Israel na Palestina yanayosimamiwa na Misri.


Katika hali kama hiyo, Palestina anazungumza na Misri na Saudi Arabia, naye Israel anazungumza na Misri na Saudi Arabia, kisha Misri anapeleka ujumbe wa walichozungumza na kupokea majibu kwa pande zote mbili.

Haya ni mazungumzo magumu kweli kuhitimishwa na kupata suluhisho la kudumu. Ni kutokana na mimi kuepuka kutumbukia katika mtego huo nachukua fursa hii kumpongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuwa mwanamke wa kwanza kuchaguliwa kwa kura kuwa Rais wa Tanzania. Hongera Rais Samia umeandika historia isiyofutika.

Sitanii, baada ya pongezi hizi zipo falsafa mbili; ya kwanza inasema; “Njia uhalalisha mwisho” na ya pili inasema; “Mwisho uhalalisha njia.” Sitajikita sana kwenye nadharia hizi, ila niruhusu tu, niseme bayana ukweli uniweke huru.

Tumefika hapa si kwa ajali, bali kutokana na matamanio ya baadhi ya wana – CCM ambao mchana walikuwa wanavaa shati la kijani, na usiku wanazunguka wakimpinga Mwenyekiti wao asigombee urais.

Ni masikitiko kuwa ubaguzi wa kijinsia, kwamba baadhi ya wana-CCM hawakuangalia uwezo wala mambo makubwa anayoyafanya Rais Samia ikiwamo ujenzi wa Bwawa la Mwalimu Nyerere na Reli ya Kisasa (SGR) ambavyo Rais Magufuli alianzisha akafariki dunia na kuacha havijakamilika, lakini Rais Samia kwa ushupavu mkubwa akaendeleza ujenzi na ununuzi wa vichwa vya treni na mabehewa, hadi sasa inafanya kazi kati ya Dar es Salaam na Dodoma.

Kipande cha Mwanza – Isaka kinakaribia asilimia 70 na ujenzi wa Dodoma – Tabora – Kigoma hadi Burundi uko katika hatua mbalimbali.

Hawa hawakuangalia ujenzi wa Daraja la Kigongo/Busisi, linaloitwa Daraja la Magufuli, ambalo Rais Samia kwa ujasiri mkubwa amelijenga, huku akijenga sambamba mradi wa Bwawa la Mwalimu Nyerere lililogharimu Sh trilioni 6.5 linalozalisha umeme Megawati 2,115 na kuifanya Tanzania kuwa na umeme mwingi kuliko nchi zote za Afrika Mashariki. Megawati 4,031, huku DRC ikiwa na Megawati 2,900, Kenya (Megawati 2,600), Uganda (Megawati 2,400), Rwanda (Megawati 406) na Burundi (Megawati 166).


Wahafidhina hawa waliokuwa hawataki mwanamke kuchaguliwa kuwa Rais, hawakuangalia kwamba kupitia fedha za Uviko – 19, Rais Samia amejenga madarasa zaidi ya 18,000 nchi nzima, vituo vya afya, hospitali, madawati, viti na meza na hadi sasa hakuna mzazi anayedaiwa kuchangia madawati au kujenga madarasa inapofika Januari, kama ilivyokuwa miaka yote.

Hawakuangalia ujenzi wa madaraja, barabara katika maeneo mbalimbali ya nchi ikiwamo Jiji la Dar es Salaam ambalo vumbi linatimka kila kona kwa ujenzi wa barabara.

Narudia, haya ni baadhi ya mambo ambayo wahafidhina hawataki kuyasikia kwani wanaona yanampa sifa Rais Samia. Mwanzoni mkakati ulikuwa kumfanya ashindwe kuyafanya haya maendeleo; achukiwe, lakini walipoona amewashinda; ametenda, wakaanza kumchimbia mashimo.

Sitanii, nimesema ukweli utatuweka huru. Tangu nchi hii imepata uhuru, vurugu za kisiasa zimekuwapo. Tuliporejesha mfumo wa vyama vingi mwaka 1992, tunafahamu wanasiasa wamekuwa wakifunguliwa kesi nyingi.

Akina Prof. Ibrahim Lipumba wa CUF, hayati Agustino Lyatonga Mrema, Leo Lwekamwa, Dk. Masumbuko Lamwai, Wilfred Lwakatare, James Mbatia, Dk. Wilbrod Slaa, Benedict Mutungilehi, Dk. Aman Walid Kabrourou, Maalim Seif Sharif Hamad, Ismali Jussa, Hamad Rashid, Freeman Mbowe, Tundu Lissu, Zitto Kabwe na wafuasi wao katika upinzani walipata kufunguliwa kesi nyingi za aina mbalimbali wakidaiwa kukiuka sheria za siasa. Hawakuuawa wala kupotezwa na watu wasiojulikana.

Sitanii, Awamu ya Tano ilipoingia madarakani chini ya Rais John Pombe Magufuli, tukaanza kusikia msamiati wa “Watu Wasiojulikana.” Tangu mwaka 2015 nchi yetu ikaanza kuonja damu. Wakapotea katika mazingira ya kutatanisha akina Ben Sanane.

Akauawa hadharani Alphonce Mawazo kule Geita. Tundu Lissu akamiminiwa risasi mchana kweupe Dodoma. Wahusika hawakupatikana wala kuchukuliwa hatua. Kidogo kidogo tukaanza kuzoea, laana ya damu aliyoisema Mwalimu Julius Kambarage Nyerere ikaanza kusambaa.

Awamu ya Sita ilianza viruzi sana. Rais Samia aliunda Kikosi Kazi. Kikosi Kazi kikatoa mapendekezo, akaruhusu siasa kufanywa hadharani kwa vyama vyote.

Tukashuhudia wapinzani wanafanya siasa, baadhi wakimwaga sera na matusi. Rais Samia akafuta kesi zaidi ya 400 zilizokuwa zinawakabili wapinzani. Akahudhuria mkutano mkuu wa Baraza la Wanawake CHADEMA (BAWACHA) pale Moshi. Umaarufu wa Rais Samia ukapanda kwa kasi. Kila mtu akamwita ‘Mama’.


Sitanii, nadhani wahafidhina ndani ya CCM hawakulipenda hili. Wakaona mpango wao wa kumzuia asigombee urais mwaka 2025 unayeyuka. Ni wazi wakamshauri na pengine wakamtia hofu, kuwa sasa wapinzani wake watamwangusha. Ndani ya CCM tunakumbuka Job Ndugai (Mungu amlaze mahala pema peponi) alivyokuwa akimsulubu Rais Samia na kilichomkuta hadi kujiuzulu. Ndugai hakuwa peke yake. Si kwamba masalia ya Ndugai yaliisha. Tumewaona wengine.

Ile ya Rais Samia kurejesha amani, haikuwafurahisha wahafidhina. Wakatafuta njia ya kumtenganisha na wananchi. Mara tukasikia Mdude Nyangali amepotea. Mara tukasikia Deus Soka na wenzake wanne wamepotea.

Mara Ali Kibao akashushwa kwenye gari pale Tegeta na mwili wake ukaokotwa amecharangwa. Hii ilikuwa mbegu ya chuki iliyopandwa makusudi. Iwe ilifanywa na wahafidhina ndani ya CCM au wapinzani kama njia ya kupandikiza chuki kwa wananchi, kwa hakika imeleta chuki.


Tumeushuhudia mnyukano na sarakasi za wana-CCM kumgeuka mwenyekiti wao hadharani akiwamo Humphrey Polepole. Kisha katika mazingira ya kuelekea karibu na uchaguzi, tukaambiwa Polepole amepotezwa. Mbegu ya chuki ikaendelea kupandwa.

Nimesema walikuwapo wakosaji wa kisiasa katika nchi hii tangu enzi za uhuru. Hata watu waliokula njama kuipindua Serikali akina Uncle Tom, mwaka 1982 bado walifikishwa mahakamani. Hawakupotezwa.

Sitanii, yeyote anayetenda matendo maovu, kuchochea wananchi, kuhamasisha vurugu, katika mkondo wa utawala wa kisheria njia sahihi ni kumfikisha mahakamani si kumalizana naye kwa kumpoteza.

Nimewataja wanasiasa wa upinzani ambao walipandishwa kizimbani mara nyingi hadi wakavifahamu viambaza vya mahakama, lakini hawakupotezwa.

Nimesema makala hii itakuwa na unayoyapenda na usiyoyapenda. Nafahamu nilipompongeza Rais Samia na kueleza makuu aliyoyatenda huenda umechukia na ukaanza kunitukana. Nimefungua kabrasha hili la utekaji na mauaji, naamini inawezekana wewe sasa unanipongeza na aliyekuwa ananipongeza hapo juu kwa kumsifia Rais Samia sasa ananimwagia matusi. Anaona nimetumwa. Mimi niko hivi miaka yote. Ukweli utatuweka huru.

Yapo mengi naweza kujaza gazeti zima, hapo juu nimesema nitagusa yanayowakera vijana. Jambo namba moja linalokera vijana ni kuona anayetoa maoni anapotea. Vijana hawataki kupotezwa katika nchi yao huru.

Wanataka asiyekubaliana na maoni wanayoyatoa atoe maoni mbadala au aende mahakamani, mahakama itoe haki kwa kumtia hatiani au kumwachia huru mtuhumiwa. Katika mchakato wa maridhiano, hili liwe namba moja. Watu wasipotee.

Suala la pili ni huduma zinazotolewa katika ofisi za umma. Watumishi wa umma wengi wamekuwa jeuri usipime. Hospitalini manesi wanatukana watu, polisi anamwambia mtu nitakuweka ndani na anamweka, wananchi wananyang’anywa ardhi zao na nyumba na watu wenye fedha na mamlaka.

Hati za watu zinabadilishwa umiliki na wahusika wanatamba. Kauli za ‘hunijui mimi’ wanasema zimerejea. Kuhamisha mwanafunzi kutoka shule moja kwenda nyingine wazazi wanadaiwa Sh 500,000 kama rushwa vinginevyo wanaambiwa nafasi hazipo.

Hospitalini daktari anaandika dawa anamwekelekeza mgonjwa duka la dawa la kwenda kununua, maduka ya manesi na madaktari yamejipanga nje ya hospitali. Ajira nafahamu Rais Samia ameajiri vijana 155,000 baada ya miaka saba iliyotanguliwa serikali kutoajiri kabisa.

Vijana wanasema wakipeleka maombi kwenye ajira portal wanapata watoto wa wakubwa (sijui hili lina ukweli kiasi gani).
Vijana wanasema ama viongozi wa umma au watoto wao wanatamba kuogelea katika utajiri kwa kuwakoga wakituma picha kwenye mitandao kuonyesha wanavyokula maisha, tena kwa lugha za kejeli.

Binafsi napenda utajiri, napenda watu kwenda kubarizi, ila lugha na mazingira ya baadhi ya viongozi au watoto wao kuwakoga watu badala ya kuonyesha kuwa wamekwenda hija kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa baraka, hii inakuwa kero kwa vijana.


Sitanii, angalau sasa tumshukuru Kamishna Mkuu wa TRA na Serikali baada ya kupitisha sheria bungeni ikizuia ofisa yeyote wa Serikali au TRA kufunga biashara ya mtu bila kibali cha waziri. Hata hivyo, ndani ya TRA bado wapo watendaji miungu watu. Pamoja na juhudi anazofanya Kamishna Mkuu, Yusufu Mwenda kuibadili TRA, bado wapo watu wenye viburi.

Unafanya makadirio tarehe 20 ya mwezi, tarehe 21 unapigiwa simu kuwa ukachukue barua ya ‘default’ (kukataa kulipa kodi) wakati fomu ya makadirio inakupatia siku 30 kuyapinga makadirio hayo unapodhani hayako sawa. Hawa wanamhujumu Mwenda na Rais Samia pia.

Katika mazingira haya, vijana wanapokutana na watumishi wa TRA wa aina hii wanaopingana na maelekezo ya Kamishna Mkuu Mwenda wakakamata mali na kuweka kufuli kwenye biashara kinyume cha sheria wanatengeneza chuki. Yapo mengi yanayowakera Watanzania, lakini mwishowe ukiwasikiliza kuna sentensi wanaitoa.

Kwamba “wanampenda Rais Samia ila anaangushwa na wasaidizi wake.” Sentensi hii nimekutana nayo mara nyingi.
Sitanii, sasa tuko hapa tulipo. Ni wajibu wetu kujiuliza tunatokaje? Nafahamu chama cha CHADEMA kina msimamo wake hadi kimesusia uchaguzi mkuu wa mwaka huu. Mara kadhaa kimeitwa mezani Ikulu na kwenye Kikosi Kazi viongozi wake wakuu wakagoma kuwa na maridhiano.

Ninalofahamu chama hiki hakiwezi kuendelea kugoma milele. Chama hiki hakina maslahi yoyote kuona maisha ya Watanzania yanapotea. Naamini kiligoma kufikisha ujumbe, na pengine maandamano yaliyogeuka uasi yamefikisha ujumbe kilioukusudia.

Sasa wakati umefika. Nafahamu katika majadiliano kuna kupata kidogo na kuachia kidogo. Najua viongozi wa CHADEMA wana kesi mahakamani. Naamini hii ni mojawapo ya ajenda ya mazungumzo katika maridhiano. Ikibainika kuwa kesi hizi zilitokana na msukumo wa kisiasa, Serikali kupitia CCM itapaswa kuangalia uwezakano wa kesi hizi kuzifuta kama awali Rais Samia alivyofuta kesi zaidi ya 400 zilizokuwa zinawakabili wafuasi wa CHADEMA.

CHADEMA nao kwa upande wao, ni wazi watapaswa kulegeza msimamo. Katika dunia ya sasa huwezi kupata kila kitu katika mazungumzo. Bahati nzuri tunayo mifano hai. Zanzibar baada ya uchaguzi wa mwaka 1995, zilitokea vurugu. Waliingia mwafaka wa kwanza uliosimamiwa na aliyekuwa Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Madola, Chifu Emeka Anyauoku wa Nigeria.

Mwaka 2001 ikatokea zahama tena, Rais Benjamin Mkapa akasimamia mazungumzo yakazaa mwafaka wa pili. Mwaka 2010 Rais Amani Abeid Karume na Maalim Seif Sharif Hamad walizungumza wakaingia mwafaka wa tatu, uliozaa Serikali ya Ummoja wa Kitaifa.

Utashangaa msomaji, wakati tumezoea vurugu za kisiasa Zanzibar katika uchaguzi, mwaka huu ukiacha maneno na msuguano wa “kura ya mapema” ilibidi Azam na kampuni nyingine za usafiri kusitisha boti, kwani zamu hii watu walikuwa wanapanda boti kukimbilia Zanzibar badala ya Wazanzibari kukimbilia Dar es Salaam. Kumbe mwafaka wa 2010 umeipiga pasi Zanzibar.
Leo nenda Zanzibar uone kasi ya maendeleo. Miaka michache ijayo, mtu akifika Zanzibar atadhani yuko Dubai. Amani inalipa.

Jirani zetu hapa Kenya, baada ya uchaguzi wa mwaka 2007, walivurugana na kuuana vilivyo. Ikabidi Mzee Mwai Kibaki na Raila Odinga waingie mwafaka. Wakaunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa. Odinga akawa Waziri Mkuu.

Alipoingia Rais Uhuru Kenyata, naye mwanzo alitaka kuwa mgumu, lakini akabaini mwafaka ndiyo salama yake. Rais William Rutto alikuwa amesema hakuna ‘nusu mkate’, lakini baadaye ikathibitika kuwa hakuna mkate mgumu mbele ya chai. Ameunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa, kwa kiasi fulani wametulia.
Amewashirikisha wapinzani.

Sitanii, kama Zanzibar wameweza Tanzania Bara inashindwa nini? Kubwa ni tuitangulize nchi yetu. Naiomba Serikali ikiongozwa na CCM kama ambavyo imekwishatamka bayana kuwa iko tayari kwa maridhiano, wakati ni sasa. Maridhiano yanatuhusu kama nchi. Tanzania inayo nafasi kubwa kiuchumi. Madini ya Lithium tuliyogundua na Nikel iliiyopo Kabanga, Ngara yanayotengeneza betri za magari ya umeme, yanawatoa roho Wazungu.


Natamani CCM na CHADEMA tukipe nafasi kizazi hiki kishuhudie utamu wa nchi kuelekea katika utajiri. Uwekezaji wa dola bilioni 42 pale Lindi kuzalisha LNG ukianza, bomba la mafuta kutoka Hoima, Uganda kuja Chongoleani, Tanga linalojengwa, ujenzi wa reli ya SGR unaoendelea utakaowezesha kwenda hadi Mwanza na Kigoma kutoka Dar es Salaam kwa saa 8. Kuunganisha nchi jirani za Burundi na DRC kwenye SGR, kujenga reli ya kisasa kutoka Tanga hadi Musoma na Songea hadi Mtwara, ni ukombozi halisi wa uchumi wa Tanzania.


Naomba sana vyama hivi na vya upinzani vingine tuzungumze nchi ipate nafasi ya kukuza uchumi, kuvutia wawekezaji, mpango wa kongani za viwanda kila wilaya na ujuzi kutoka vyuo vya VETA ni ukombozi halisi. Narudia, inawezekana katika makala hii sijakufurahisha, lakini basi chagua angalau moja kati ya niliyoyasema, ushiriki kuhamasisha maridhiano nchi yetu amani itamalaki.

Sitanii, ukiwa na hasira usifanye uamuzi na ukiwa na furaha usitoe ahadi. Najua kila mtu anayo dhambi yake. Iwe uko chama tawala, serikalini au kwenye upinzani, kuna aina ya dhambi uliyonayo na wewe unaifahamu vyema kuliko mimi. Basi tukumbuke maneno ya Yesu Kristu, kwamba “Sikuja kuwaita watu wema, bali wenye dhambi wapate kutubu.” Tusameheane, tulijenge taifa letu, tulipofika tusisonge mbele zaidi. Mchakato wa maridhiano uanze haraka. Kwa vyovyote iwavyo, jukumu hili liko mikononi mwa Rais Samia.

Mungu ibariki Tanzania.

0784 404 827