Na Deodatus Balile, JamhuriMedia, Mwanza

Leo tumechapisha toleo maalumu. Toleo hili ni la watia nia waliopitishwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM). Yapo majina makubwa yaliyoachwa kama Mbunge wa Bumbuli, January Makamba; Mbunge wa Kisesa, Luhaga Mpina na wengine wengi. Lakini pia wapo walioruka dirishani wakati treni inatembea, akiwamo aliyekuwa Balozi wa Tanzania nchini Cuba, Humphrey Polepole.

Sitanii, ipo misemo miwili maarufu hapa nchini ilisemwa na Mwalimu Julius Nyerere. “Nchi yetu haina dini,” na “Ikulu ni mahala patakatifu.”

Wiki moja iliyopita niliandika makala kuhusu Polepole nikasema huyu kijana “ni sikio la kufa”. Katika makala ile nilieleza mengi, ikiwamo hoja yake anayodai kuwa utaratibu ulikiukwa jinsi ya kumpata Rais Samia Suluhu Hassan kama Rais wa Tanzania baada ya kifo cha Rais John Pombe Magufuli, na mgombea urais wa CCM 2025. Lakini Rais Samia alipomteua Polepole kuwa Balozi wa Tanzania nchini Cuba, hapo utaratibu haukukiukwa!

Mimi ni muumini wa utawala wa sheria, maana ukitawala kwa mujibu wa sheria unakuwa na utawala bora. Nilifafanua na ni kitu ambacho kipo wazi kuwa Ibara ya 37(5) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, inasema ikitokea Rais aliyeko madarakani akafariki dunia, basi Makamu wa Rais anaapishwa kushika madaraka katika kipindi kilichosalia. Ibara hii inapaswa kusomwa sambamba na Ibara ya 40(4) ya Katiba ya Tanzania (1977).

Kwa kuwa Polepole anaonekana kuupotosha umma kwa makusudi, akijenga hoja kuwa kwa utamaduni wa nchi yetu mtu akishakuwa Makamu wa Rais hastahili kuwa Rais wa Tanzania, lakini kama hiyo haitoshi, inanishangaza kuona kuna watu wanaamini anachosema Polepole wakidhani ni cha kweli, hivyo wanamshangilia, imenipasa niliandike tena hili. Ibara hizo zinasema hivi:

“37(5) Endapo kiti cha Rais kitakuwa wazi kutokana na Rais kufariki dunia, kujiuzulu, kupoteza sifa za uchaguzi au kutomudu kazi zake kutokana na maradhi ya mwili au kushindwa kutekeleza kazi na shughuli za Rais, basi Makamu wa Rais ataapishwa na atakuwa Rais kwa muda uliobaki katika kipindi cha miaka mitano na kwa masharti yaliyoelezwa katika ibara ya 40, kisha baada ya kushauriana na chama cha siasa anachotoka Rais atapendekeza jina la mtu atakayekuwa Makamu wa Rais na uteuzi huo utathibitishwa na Bunge kwa kura zisizopungua asilimia hamsini ya wabunge wote.”

Ibara ya 40(4) inasema: “Endapo Makamu wa Rais anashika kiti cha Rais kwa mujibu wa masharti ya ibara ya 37(5) kwa kipindi kinachopungua miaka mitatu ataruhusiwa kugombea nafasi ya Rais mara mbili, lakini kama akishika kiti cha Rais kwa muda wa miaka mitatu au zaidi ataruhusiwa kugombea nafasi ya Rais mara moja tu.”

Ukizisoma kwa pamoja hizi Ibara mbili, na ukakumbuka kuwa Rais Samia ameingia madarakani kwa mujibu wa Ibara ya 37(5) Machi 19, 2021, basi kufikia Oktoba, 2025 atakuwa ameshika madaraka kwa zaidi ya miaka mitatu. Kwa mantiki hiyo, anaruhusiwa kugombea kipindi kimoja tu, yaani 2025 – 2030. Hapo ndipo baada ya hiyo miaka mitano, Katiba inamzuia kugombea tena nafasi hiyo.

Sitanii, baada ya kuandika makala hiyo Polepole nina uhakika asilimia 100 kuwa ameisoma, ila bado naona anaendelea kutoa maelezo yasiyokuwa na msingi wa kisheria wa kanuni yoyote katika nchi hii.

Kwa muktadha huo, nashawishika kuamini maneno ya Mwalimu Julius Nyerere kuwa inawezekana Polepole anatumia kila mbinu kupata nafasi ya kuingia Ikulu, ila anaona Rais Samia ni kisiki kwake kufikia malengo hayo.

January Makamba na Luhaga Mpina wana haiba tofauti. Wakati Mpina hakuwa akiona tabu kulaza kichwa chake katika tairi la treni inayotembea, January yeye alitumia mbinu za porini. Ilielezwa, lakini naye mara kadhaa alitamka kuwa angalau urais si sasa, bali kuelekea 2030. Zipo taarifa za wapambe wake ambazo sauti zilivuja mtandaoni wakimbeza Rais Samia na kumsifia Makamba.

Kimsingi Makamba analo kundi ambalo kupitia uteuzi huu, wafuasi wake kadhaa wamebaki pembeni. Wachache wamepenya, lakini ukiwaangalia ushindani ulioko majimboni mwao, ni ile ambayo ukimwona mbuzi anakimbilia jikoni, unamwacha akafie kwa muuza supu. Kura za maoni zinayo nafasi ya kutushangaza kwa hao waliopenya.

Sitanii, ninaandika makala hii kwa nia ya kuwarekebisha wanasiasa wanaokuwa na tamaa zinazofifisha maono. Leo ingekuwa Rais Samia hajajenga Bwawa la Mwalimu Nyerere likakamilika, ingekuwa hajajenga SGR ikaanza kazi na kuanza vipande vikubwa zaidi, ingekuwa hajasogeza maji vijijini, umeme wa REA ungekuwa haujafika kila kijiji, sijui wakubwa hawa wangemsemaje?

Rais Samia ametenda kwa uadilifu. Ukiangalia katika afya, elimu, amewapa watu nafasi katika uongozi na akawa anatamka bayana kuwa anayafahamu makundi ya wahusika, ila wote amewaunganisha. Kwa bahati mbaya, narudia, kwa bahati mbaya nadhani baadhi ya wakubwa hawa wamemkadiria vibaya Rais Samia. Wamemchukulia kuwa ni mwanamke, hivyo wakadhani watamburuza.

Wapo waliokuwa na ujasiri wa kutamka kuwa bila wao Baraza la Mawaziri haliwezi kwenda. Wamekaa nje ya Baraza na kila kitu kimekwenda vizuri. Leo tunakweda kwenye kura za maoni zinazopaswa kutumika kama kipimo. Zitumike kuchagua wagombea wanaojitambua. Wagombea wenye malengo binafsi wapewe kisogo.

Kwa vyovyote iwavyo, tujue Tanzania ni moja. Mnapotetea nafasi zenu, mjue amani, umoja na mshikamano vinapaswa kubaki kuwa nguzo inayotupatia heshima sisi Watanzania. Hakuna anayezuiwa kuzungumza lolote, ila uwasilishaji uwe wa staha.

Lugha ni muhimu katika kufikisha ujumbe. Wagombea muwashawishi wananchi kuwachagua, ila msisahau kuwa lengo kuu ni kuwatumikia wao, si mbio za urais siku za usoni. Watanzania tukiridhika na tulichonacho, makubwa yatakuja kwa neema za Mungu. Mungu ibariki Tanzania.

0784 404 827