Na Deodatus Balile, JamhuriMedia, Dodoma
Mwaka jana niliposikia tetesi kwamba kuna kundi linaamini Rais Samia Suluhu Hassan anapaswa kuongoza kipindi kimoja na kuishia mwaka 2025, sikuzipa uzito. Niliwaza kuwa huenda ni zile kamati za fitina ndani ya vyama vya siasa, pengine zinalenga kuchangamsha siasa.
Januari 19, 2025 nilikuwapo pale Ukumbi wa Jakaya Kikwete – Dodoma. Nikashuhudi mchakato wa uteuzi wa Mgombea Urais wa CCM, Dk. Samia Suluhu Hassan, Mgombea Urais wa Zanzibar, Dk. Hussein Ali Mwinyi na Mgombea Mwenza wa Rais Samia, Balozi Dk. Emmanuel Nchimbi.
Sitanii, baada ya mkutano huo nilianza kusikia manung’uniko kwa baadhi ya viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM). Kada wa CCM, Mchungaji Godfrey Malisa wa Moshi yeye alikuja hadharani kupinga mchakato wa uteuzi wa Rais Samia na wenzake kuwa wagombea wa CCM katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.
Baadaye akajitokeza Mbunge wa Kawe, Mchungaji Josephat Gwajima. Mbunge wa Kisesa, Luhanga Mpina – huyo tulikwishazoea kauli zake.
Hivi karibuni amejitokeza Balozi wa Tanzania nchini Cuba, Humphrey Polepole. Akajiuzulu ubalozi. Mwanzoni akaanza na hoja ya kupinga mchakato wa uteuzi wa Rais Samia, akisema umekiuka taratibu za chama. Julai 19, 2025 akaitisha alichokiita mkutano na waandishi wa habari, akiwa kwenye chumba peke yake, hivyo akafanya mkutano kwa njia ya mtandao.
Sitanii, alizungumza mengi aliyoyaita asilimia 25 ya anacholenga kuzungumza, ila akahama katika hoja yake ya msingi ya kukiuka utaratibu wa mchakato wa uteuzi, kwa kinywa chake akathibitisha kilichokuwa kinavuma kwa kusema: “Rais Samia huyu mwisho ni 2025”. Sentensi hiyo ikanipa jibu la Polepole na kundi lake wanalenga nini. Kitambo niliambiwa kuna mtandao unajiita Sukuma Gang.
Nilielezwa na hata siku moja wakati Rais Samia anahutubia alielekea kugusia hili. Kundi hili naambiwa halikutaka Rais Samia aapishwe kuwa Rais wa Tanzania kwa mujibu wa Ibara ya 37(5) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Uvumi huu ilikuwa nimeusikia awali kwa kasi kubwa Machi 17, 2021. Niliamshwa saa 7 usiku Machi 17 kuamkia Machi 18, 2021, nikaambiwa moto unawaka.
Sitanii, kama mwanahabari na mwanasheria, niliamua kufanya mahojiano na Shirika la Utangazaji la Taifa (TBC) kukata mzizi wa fitina. Ukiingia kwenye mtandao wa YouTube, utaona kipindi cha Jambo kinachorushwa asubuhi na TBC, asubuhi ya Machi 18, 2021 nilihojiwa na Mkurugenzi Mkuu wa TBC, Dk. Ayubu Rioba. Kati ya aliyonihoji Dk. Rioba ni utaratibu unakuwaje iwapo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania anafariki dunia akiwa madarakani.
Nilijibu swali lake kwa kusoma Ibara ya 37(5) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayosema: “Endapo kiti cha Rais kitakuwa wazi kutokana na Rais kufariki dunia, kujiuzulu, kupoteza sifa za uchaguzi au kutomudu kazi zake kutokana na maradhi ya mwili au kushindwa kutekeleza kazi na shughuli za Rais, basi Makamu wa Rais ataapishwa na atakuwa Rais kwa muda uliobaki katika kipindi cha miaka mitano na kwa masharti yaliyoelezwa katika ibara ya 40, kisha baada ya kushauriana na chama cha siasa anachotoka Rais atapendekeza jina la mtu atakayekuwa Makamu wa Rais na uteuzi huo utathibitishwa na Bunge kwa kura zisizopungua asilimia hamsini ya wabunge wote.”
Baada ya mahojiano haya, nilipata simu ya mtu mmoja, aliyesema: “Asante sana Balile. Umemaliza ubishi. Kuna watu walikuwa wanapendekeza Makamu wa Rais Samia aapishwe kuwa Kaimu Rais na baada ya mazishi twende kwenye uchaguzi”
Nilitajiwa majina ya hata watu waliokuwa wanasoma Katiba ya zamani kabla ya marekebisho ya 14 ya mwaka 2005, waliodhani wao ndio wanaopaswa kushika madaraka iwapo Rais atafariki dunia.
Sitanii, ninyi nyote mlikuwapo mnakumbuka mmoja wa viongozi alivyoanza kumsulubu Rais Samia baada ya kuwa ameapishwa. Mnakumbuka wana – CCM wenzake walimshukia kiongozi huyo kama mwewe, akalazimika kuandika barua ya kujiuzulu kwa mwandiko wa herufi kubwa. Kundi hili halijawahi kufa. Kundi hili halijawahi kupotea. Bado linaamini lenyewe ndilo linastahili kushika madaraka ya urais, kumbe sivyo.
Polepole huyu ni sikio la kufa. Najiuliza huyu Polepole haisomi Katiba ya CCM? Katiba ya CCM Ibara ya 100 (2) inasema: “Mkutano Mkuu wa CCM wa Taifa utakuwa ndicho kikao kikuu cha CCM kupita vyote na ndicho kitakachokuwa na madaraka ya mwisho.
Ibara ya 101(5)(b) inasema kazi za Mkutano Mkuu wa CCM ni pamoja na: “Kuchagua jina moja la mwanachama mmoja atakayesimama katika uchaguzi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.” Kinachonipa shida, huyo Polepole sehemu kubwa ya watu anaohusishwa nao kwenye hili vuguvugu walikuwapo kwenye Ukumbi wa Jakaya Kikwete pale Dodoma Januari 19, 2025.
Pale ukumbini baada ya hoja ya kumteua Rais Samia kuwa mgombea urais wa CCM, Balozi Dk. Nchimbi kuwa Mgombea Mwenza (Makamu wa Rais) na Dk. Hussein Mwinyi kuwa mgombea wa CCM Zanzibar, sikushuhudia hata mtu mmoja akinyoosha kidole kupinga uamuzi huu. Sana sana Mpina ndiye niliona picha yake akiwa amekaa chini wakati wajumbe wenzake wanashangilia uteuzi huu.
Sitanii, kama si unafiki ilikuwaje siku ya mkutano hakuna aliyejitokeza kupinga ibara hizo mbili zilizotumika katika Mkutano Mkuu wa CCM kufanya uteuzi huu na sasa wajimwaye hadharani kuwa hawaukubali? Hili si jambo jepesi. Ninafahamu wengine hawampingi Rais Samia kwa lolote, bali kwa jinsia yake. Mfumo dume umewakolea vichwani kwa kiwango ambacho wamepofushwa.
Wamepofushwa, hawaoni hata mambo makubwa aliyoyafanya kama ujenzi wa Bwawa la Mwalimu Nyerere, ukamilishaji wa SGR kati ya Dar – Dodoma na kuanzisha ujenzi wa Dodoma – Tabora – Kigoma na Tabora – Mwanza. Hawaoni madarasa na shule zilizojengwa, upatikanaji wa maji, vituo vya afya na kubwa kuliko yote, amani iliyotamalaki, ambayo leo hauamki asubuhi ukakuta watu wanafunguliwa kesi za kijinga Mahakama ya Kisutu.
Polepole huyu huyu ambaye leo baadhi ya watu wanamshangilia, ndiye aliua mfumo wa upinzani nchini, akiasisi mchezo wa kuonyesha kuwa wapinzani hawajui kujaza fomu za uchaguzi mwaka 2020, wakaenguliwa wote. Ni Polepole huyu huyu aliyekuwa anarukaruka kwenye zuria jekundu, akituasa tusipingane na mamlaka mwaka 2020, huku akitukoga kwa utajiri wake, akihoji kama tunaijua V8, huku yeye akiitia v-Eighty!
Watanzania tusiwe wepesi wa kusahau. Akiwa Katibu Mwenezi wa CCM kwa uteuzi wa bosi wake, Mtanzania mwenzetu, Alphonce Mawazo, aliuawa kule Geita, Polepole hakutia neno. Mohamed Dewji (Mo) alitekwa, Polepole hakutia neno. Msamiati wa watu wasiojulikana uliasisiwa na amani ikapotea nchini, mtandao ambao masalia yake yameendelea kusumbua kwa baadhi ya nyakati hata sasa, Polepole hakutia neno.
Sitanii, kijana huyu historia yake si safi kihivyo. Ukitaka kufahamu zungumza na wagombea mwaka 2020 alivyowatenda waliokuwa na hamu ya kupata nafasi za ubunge na udiwani au kuteuliwa katika nyadhifa mbalimbali. Watanzania tusifanywe mazezeta. Polepole nadhani sasa anatafuta akamatwe kisha ayatangazie mataifa kuwa amekamatwa kwa kutetea haki.
Kwa vyovyote vile, ana nia ovu. Aliyekuwa Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Marekani, Hilary Clinton, alisema “Kioo cha dari ni kigumu, lakini angalau nimekitia nyufa.”
Kuna kila dalili Rais Samia kwa alipofikia kioo hiki cha mfumo dume hataishia kukitia nyufa tu, bali atakipasua na kusonga mbele. Hili Polepole na wenzake hawalipendi. Walijaribu mwanzoni wakakwama, nadhani sasa wanajaribu maji kwa miguu yote miwili, bila kujua urefu wa kina cha maji yenywe.
Nihitimishe makala hii kwa maneno aliyoniambia mmoja wa wananchi wa kawaida wakati tunajadiliana suala hili: “Mama huyu, Mungu ambariki. Leo TRA wanakusanya kodi hadi Sh trilioni 3, bila kumtia mtu pingu au kufunga biashara yoyote ya mtu. Mama huyu ana nia njema na taifa letu. Ajipe moyo, hawa wanaomtafuta, wataishia kulia na kusaga meno, na yeye atalitumikia taifa letu hadi mwaka 2030.” Mungu ibariki Tanzania.
0784 404 827