Na Abdallah Amiri, JamhuriMedia, Igunga

Jeshi la Polisi Mkoa wa Tabora,limemfukuza kazi askari wake Koplo Gebasa G. 8265.

Askari huyo alikuwa akifanya kazi kituo kidogo cha Polisi Kata ya Sungwizi Tarafa ya Simbo Wilaya ya Igunga.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora, Kamishina Msaidizi, Richard Abwao amethibitisha kufukuzwa kwa askari huyo.

Kamanda Abwao amesema uamuzi wa kumfukuza kazi askari huyo umekuja baada ya kufanya uchunguzi wa kina kutokana na tuhuma iliyokuwa ikimkabili ya kumbaka mwanafunzi wa kidato cha pili Februali 22, 2025.

Amesema siku ya tukio majira ya saa 3:30, usiku katika uwanja wa mpira jirani na Shule ya Sekondari Nkinga, askari huyo alituhumiwa kumbaka mwanafunzi wa kidato cha pili mwenye umri wa miaka 16 ambaye jina lake limehifadhiwa.

Amesema baada ya Jeshi la Polisi kupata taarifa hiyo, walimkamata askari huyo, kisha kumuweka mahabusu ambapo uchunguzi ulifanyika kwa kina na kubaini askari huyo alishindwa kutekeleza majukumu yake ya kazi, badala yake alijihusisha na kitendo hicho.

“Mimi kama kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora, nimefanya hivyo ikiwa ni moja ya majukumu yangu ya kusimamia nidhamu ya askari wote.

“Napenda kutoa onyo kali kwa askari yoyote atakaye bainika kufanya upuuzi kama huo hatutasita kumfukuza kazi,huku akitoa onyo pia kwa baadhi ya wananchi wenye tabia hiyo kuacha mara moja kwa kuwa watakaobainika nao watakamatwa na kufikishwa mahakamani.”

Nao baadhi ya wananchi wa Kata ya Sungwizi na Nkinga, Ramadhani Juma, Adija Mussa, Issa Shabani, Rehema Sudi, kwa nyakati tofauti wamemshukuru Kamanda Abwao kwa hatua aliyochukua ya kumfukuza kazi askari huyo.

“Kwa kweli sisi wananchi tunashukuru sana kwa hatua aliyochukua kamanda wetu Abwao kwani askari huyo amekuwa kero kwa wazazi wanaosomesha watoto wao katika shule hiyo ya sekondari Nkinga.”

Aidha wananchi hao waliomba askari huyo afikishwe mahakamani na sio kufukuzwa kazi tu kwani ushahidi upo wa kutosha. Ambapo itakuwa fundisho kwa wale wote wenye kukatiza ndoto za wanafunzi kuendelea na elimu.