Na Dotto Kwilasa, Jamhuri Media, Dodoma

Jeshi la Polisi mkoa wa Dodoma limewaomba wakazi wa mkoa huo kushirikiana kwa kutoa taarifa za watu wanaoshukiwa kuwa na viashiria vya uhalifu ili kusaidia kuwadhibiti mapema kabla hawajatekeleza vitendo vya kihalifu.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, George Katabazi, ametoa wito huo alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mafanikio ya msako wa wahalifu katika maeneo mbalimbali ya mkoa huo.

Kwa mujibu wa Kamanda Katabazi, watuhumiwa wanne wanashikiliwa kwa tuhuma za kupatikana na silaha kinyume cha sheria katika wilaya za Dodoma Mjini na Mpwapwa.

Ameeleza kuwa mnamo Mei 17, 2025 majira ya saa 10:00 jioni, katika mtaa wa Kikuyu Mission jijini Dodoma, watu wawili wakazi wa eneo hilo walikamatwa wakiwa na bastola yenye risasi 13.

Katika tukio jingine, Kamanda Katabazi amesema mnamo Mei 19, 2025 saa 11:00 jioni, katika mtaa wa Lukole wilayani Mpwapwa, walikamatwa watu wawili wakiwa na silaha ya kienyeji aina ya Shortgun iliyokatwa mtutu na kitako pamoja na risasi tano.

Aidha, Mei 18, 2025 saa 4:40 usiku, katika mtaa wa Mbuyuni, Kata ya Kizota, walikamatwa Nestory Kimario (38) na Thomas Paschal maarufu kwa jina la Sigan (28), wakazi wa Mbabala, wakiwa na mafuta ya dizeli lita 2,420 yaliyohifadhiwa kwenye madumu 89 ndani ya gari aina ya Toyota lenye namba T273 BKB.

Katika msako huo, polisi pia wamekamata vifaa mbalimbali vinavyodhaniwa kutumika kuvunjia, pamoja na runinga sita na redio saba ambazo zinadaiwa kuwa ni mali za wizi.

Kamanda Katabazi amesisitiza kuwa ushirikiano wa wananchi ni muhimu katika mapambano dhidi ya uhalifu na amewahakikishia wakazi wa Dodoma kuwa jeshi la polisi litaendelea kuchukua hatua kali dhidi ya wahalifu.