Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linaendelea na uchunguzi wa tukio la tarehe 02 Mei, 2025 la kuvamiwa na kujeruhiwa kwa Mpaluka Said Nyagali maarufu Mdude Mfuasi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo [CHADEMA] na watu wasiofahamika na kisha kutoweka naye kusikojulikana. 

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Jeshi la Polisi Mbeya imesema kuwa katika hatua za awali, Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya lilitoa wito kwa mtu yeyote mwenye taarifa za mahali alipo Mpaluka Said Nyagali maarufu Mdude azitoe ili kufanikisha kumpata pamoja na taarifa za watu waliohusika katika tukio hilo ili waweze kukamatwa.

Hivi karibuni wakati Jeshi la Polisi likiwa linaendelea na uchunguzi wa tukio hilo, wamejitokeza baadhi ya watu na viongozi wa CHADEMA na kutoa matamko mbalimbali ikiwemo kutaja baadhi ya majina ya Askari wakiwatuhumu kuhusika na tukio hilo bila kuwasilisha ushahidi wowote. 

Kufuatia kauli na matamko hayo, Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linatoa onyo kali kwa mtu au kikundi chochote cha watu wenye nia ovu kutojaribu wala kuthubutu kujihusisha na uhalifu wa aina yoyote ikiwemo kudhuru Askari ama familia za Askari. Vile vile, kabla ya kufikiria kufanya hivyo, wajionye sana na wasifikiri kufanya kitendo hicho ni rahisi kwao.

Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya halitasita kumchukulia hatua za kisheria na kumshughulikia mtu au kikundi chochote cha watu watakaojaribu kufanya uhalifu kutokana na matamko au kauli hizo zinazotolewa.