Polisi Uganda imesema imemkamata mbunge na afisa mwandamizi wa chama kikuu cha upinzani, National Unity Platform (NUP), kwa tuhuma za kuhusika katika vurugu za uchaguzi ambazo zilisababisha vifo vya takriban watu saba.

Mbunge huyo, Muwanga Kivumbi, ambaye pia ni makamu wa rais wa NUP, anadaiwa kuhusika na machafuko yaliyotokea baada ya uchaguzi.

Polisi imethibitisha kukamatwa kwa Kivumbi kupitia chapisho kwenye mtandao wa kijamii wa X, na kusema kuwa mbunge huyo atafikishwa mahakamani mara baada ya uchunguzi kukamilika.

Chama hicho kinaongozwa na mwanamuziki maarufu aliyeingia kwenye siasa, Bobi Wine, ambaye amekuwa mafichoni tangu wiki iliyopita kutokana na kile anachodai kuwa ni vitisho na ukandamizaji kutoka kwa vyombo vya usalama.

Bobi Wine, ambaye jina lake halisi ni Robert Kyagulanyi, amesema alilazimika kukimbia makaazi yake baada ya jeshi kuvamia nyumba yake saa chache kabla ya Rais Yoweri Museveni kutangazwa mshindi wa uchaguzi wa urais uliofanyika Januari 15.

Wine ameyapinga matokeo hayo, akidai kulikuwa na visa vya ukiukwaji mkubwa wa haki za wapiga kura na matumizi ya nguvu kupita kiasi dhidi ya wafuasi wake.