Na Allan Kitwe, JamhuriMedia, Tabora
JESHI la Polisi Mkoani Tabora linawashikilia watu wanne kwa tuhuma za ujambazi na mauaji ya waendesha bodaboda yaliyokuwa yakiripotiwa mara kwa mara katika maeneo mbalimbali mkoani hapa.
Hayo yamebainishwa jana na Mkuu wa Mkoa Paul Matiko Chacha alipokuwa akizungumza na Wadau wa Maendelea na Wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa.
Amesema kuwa kukamatwa kwa watuhumiwa hao kumetokana na operesheni maalum iliyofanywa na askari wa Jeshi la Polisi Mkoani hapa kwa kushirikiana na Vyombo Vingine vya Ulinzi na Usalama.
Amedokeza kuwa msako huo ulilenga kunasa wahalifu wote waliokuwa wakijihusisha na vitendo hivyo ambavyo vimekuwa vikisababisha taharuki kubwa miongoni mwa jamii na hususan waendesha bodaboda.
‘Kukamatwa watuhumiwa hawa ni hatua moja, uchunguzi bado unaendelea ili kubaini mtandao mzima na kukamata wahusika wote ili kukomesha tabia hii na hatua kali zitachukuliwa dhidi ya wahusika wote’, ameeleza.
Aidha ameongeza kuwa watu wengine wawili wanashikiliwa na Jeshi la Polisi Mkoani hapa akiwemo Kiongozi wa Serikali ya Mtaa kwa tuhuma za kuhusika na mauaji ya wanandoa wawili walioripotiwa kupotea Januri 7 mwaka huu
Ameeleza kuwa wanandoa hao ambao ni mke na mume, wakazi wa Kijiji cha Nata Kata ya Miguha Wilayani Nzega waliripotiwa kupotea katika mazingira ya kutatanisha na taarifa ilipofika Polisi uchunguzi ulianza mara moja.
Baada ya uchunguzi wanandoa hao walikutwa wamefariki na kuzikwa ndani ya jiko la nyumba waliyokuwa wakiishi, tukio hili linahusishwa na mgogoro wa kifamilia uliokuwepo.
Chacha amewataka wananchi kuendelea kutoa ushirikiano kwa vyombo vya dola kwa kutoa taarifa sahihi zitakazosaidia kukamatwa wahusika na kudhibiti uhalifu na kulinda amani ya wakazi wa Mkoa huo.


