Na George Binagi, Mwanza
Mkurugenzi wa Shirika la Afya Duniani (WHO), Prof. Mohamed Janabi amezindua wodi ya kwanza na ya kisasa nchini kwa ajili ya watoto njiti, iliyojengwa katika Hospitali ya Wilaya ya Kwimba mkoani Mwanza.
Prof. Janabi amefanya uzinduzi huo jumamosi Februari 28, 2028 kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa WHO, Dkt. Tedros Ghebreyesus ambapo ujenzi wake umegharimu shilingi bilioni 2.125 ikijumuisha jengo, vifaa tiba na mbili nyumba za watumishi.
Prof. Janabi ametumia fursa hiyo kuipongeza taasisi ya Doris Mollel (Doris Mollel Foundation- DMF) kwa kushirikiana na wadau mbalimbali ikiwemo Taasisi ya Keep a Child Alive (KCA) na Shirika la JHPIEGO kwa kufanikisha mradi huo utakaosaidia kuzuia vifo vya wazazi na watoto hasa wanaozaliwa kabla ya wakati ama chini ya uzito.
“Kila mwaka Kanda ya Afrika inapoteza watoto milioni hivyo WHO tutaendelea kuunga mkono jitihada hizi ili kuhakikisha hakuna mtoto ama mzazi anapoteza maisha” amesema Prof. Janabi huku pia akiipongeza Serikali ya Tanzania kwa jitihada inazoendelea kuchukua kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo katika kuboresha huduma za afya.
Mkurugenzi wa DMF, Doris Mollel amesema wazo la ujenzi wa wodi hiyo lilianza mwaka 2021 taasisi hiyo ilipoenesha kampeni ya kuchangia vifaa tiba kwa ajili ya wodi za watoto njiti nchini ambapo Wilaya ya Kwimba ilibainika kuwa kwenye uhitaji wa wodi na hivyo kuanza mchangato wa kutafuta fedha zilizofanikisha kukamilisha mradi huo.

Naye Mkurugenzi wa Shirika la JHPIEGO Tanzania, Alice Christensen amesema kukamilika kwa wodi hiyo kutatoa mfano kote nchini namna wodi za watoto njiti zinavyopaswa kuwa hatua itakayosaidia kuokoa maisha ya mama na mtoto wakati wa kujifungua ambapo shirika hilo limechangia zaidi ya shilingi milioni 200 kwenye utekelezaji wa mradi huo.
Kwa upande wao baadhi ya wakazi wa Kwimba akiwemo Modesta Malashi, Vumilia Ally na Mariam Lucas wamesema wodi hiyo itawaondolea adha ya kubanana kwenye wodi ya pamoja iliyokuwepo awali hospitalini hapo huku pia wakilazimika kusafiri umbali mrefu hadi Bugando inapotokea changamoto ya kujifungua.












