Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Prof. Palamagamba Kabudi, amesema kuwa serikali imekuwa ikitambua mchango wa vyombo vya habari kwa muda mrefu, tangu enzi za Mwalimu Nyerere.

Alibainisha kuwa chini ya serikali ya sasa, uhuru wa vyombo vya habari umeimarika kwa kiasi kikubwa, na hali hiyo imechangiwa na ushirikiano wa karibu kati ya wizara na wadau wa habari.

Prof. Kabudi alitaja kuanzishwa kwa Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari kuwa ni sehemu ya juhudi za kuiboresha sekta hiyo na kulinda maadili ya uandishi.

Wakati huo huo, Katibu Mkuu wa Wizara hiyo na Msemaji Mkuu wa Serikali, Bw. Gerson Msigwa, alisisitiza kuwa kwa kuwa mwaka 2025 ni mwaka wa uchaguzi, wizara iliona umuhimu wa kukutana na wadau wa habari ili kuhakikisha waandishi wanashiriki kwa maana na kwa weledi katika zoezi hilo muhimu kwa taifa.

Alisisitiza umuhimu wa kuamini uandishi wa habari kufanywa na wataalamu wenye sifa na maadili madhubuti, kama njia ya kuepuka migawanyiko isiyo ya lazima na kulinda heshima ya sekta ya habari.