Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam
Serikali inakusudia kujizatiti kuongeza mitaala zaidi ya elimu ya afya ili kuzalisha wataalamu wa afya, lakini pia kuimarisha ushirikiano wa kikanda na kimataifa katika kufanya tafiti na kutoa huduma za afya.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda ametoa kauli hiyo leo Mei 23, katika uzinduzi wa Awamu ya Pili ya Mradi wa Kituo cha Umahiri wa Magonjwa ya Moyo na Mishipa ya Damu Afrika Mashariki uliofanyika Kampasi ya Mloganzila, Dar es Salaam.
Prof Mkenda amesema mradi huo unaotekelezwa na Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) umegharimu Sh bilioni 224 fedha za mkopo wa masharti nafuu kutoka Benki ya Maendeleo Afrika (AfDB).
“Kukamilika kwa mradi huu kutapunguza utegemezi wa matibabu nje ya nchi, lakini pia mradi huu utakuwa kitovu cha utalii wa tiba na kuongeza fedha za kigeni,” ameleeza Prof Mkenda.
Kwa kutambua ukubwa wa tafiti zinazofanywa na MUHAS, Prof Mkenda amesema serikali itaangalia namna ya kuongeza bajeti ili kuwezesha uzalishaji wa tafiti hizo, lakini kutoa msukumo kwenye sayansi.
Makamu Mkuu wa MUHAS, Profesa Appolinary Kamuhabwa ametaja madhumuni ya kituo hicho kuwa ni kupunguza magonjwa na vifo vinavyotokana na moyo hasa katika ukanda wa Afrika Mashariki.

Prof Kamuhabwa amesema ili kutimiza azma hiyo, MUHAS imejipanga kutoa mafunzo, kuboresha huduma na kufanya tafiti hata hivyo hatua hiyo itasaidia kuongeza ajira.
“Sisi kama chuo lengo ni kutoa wataalamu wabobezi kwenda kutoa huduma katika vituo vya afya kotye nchini,” amesema Prof Kamuhabwa.
Sambamba na hayo, Prof Kamuhabwa ameishukuru Benki ya AfDB kwa kuendelea kuwaunga mkono katika utekelezaji wa mradi huo, lakini pia ni sehemu ya juhudi za Rais Samia Suluhu Hassan.
Aidha, Mwenyekiti wa Baraza la MUHAS, Marsha Macatta- Yambi amesema hatua ya uzinduzi wa mradi huyo inashiria kusudio la muda mrefu wa kuwa na jengo la magonjwa ya moyo awamu ya pili baada ya awamu ya kwanza kukamilika.
“Tufahamu kwamba katika ukanda huu, Muhas tumeweza kupata nafasi ya kuwa na kituo cha umahiri wa magonjwa ya moyo, na sio tu tutafaidisha watanzania, lakini tutatoa wataalamu mahiri na kujumuisha teknolojia inavyoelekea,” amesema.

Amesema upatikaji wa fedha kutoka Benki ya Maendeleo utaendelea Afrika utaendelea kuwapa hatua kubwa ya kutimiza ndoto za wanasayansi.
Awali akizungumza Mkurugenzi wa Elimu ya Juu kutoka Wizara ya Elimu, Sanyansi na Teknolojia Profesa Peter Msofe alisema matarajio ya mradi huo kwa miaka mitano ijayo ni kuwa na hospitali ya kisasa ya kufundisha inayotoa huduma za umahiri wa kinga, tiba na ukarabati wa magonjwa ya moyo na mishipa ya damu.
H
Lakini pia kusomesha wataalamu 120 katika fani mbalimbali za sanyansi, magonjwa ya moyo na mishipa ya damu na kutoa ufadhili kwa wanafunzi 20 kusomea masomo ya sayansi ya magonjwa ya moyo na mishipa ya damu.
Aidha, madhumuni ya mradi huo ni kufundisha wataalamu mabingwa na wabobezi katika sayansi ya magonjwa ya moyo, mishipa ya damu na kutengeneza mitaala.
Pia kuimarisha uwezo wa taasisi katika kutoa mafunzo, kufanya tafiti za kina kuhusu kinga, tiba na ukarabati wa magonjwa ya moyo.

