Na Mwandishi Wetu
WAZIRI wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda, amesisitiza kuwa ushiriki wa Wanawake na Wasichana katika sayansi ni nyenzo muhimu ya maendeleo ya Taifa kiuchumi, na kwamba Serikali inaendelea kuwekeza ili kuongeza wataalam katika nyanja hiyo.
Prof. Mkenda alitoa kauli hiyo jijini Dodoma katika Maadhimisho ya Siku ya Wanawake na Wasichana katika Sayansi, akieleza kuwa sayansi ni msingi wa maendeleo kwani huongeza tija katika uzalishaji na kutoa suluhisho la changamoto mbalimbali kijamii kupitia tafiti na matumizi ya teknolojia.
“Takwimu zinaonesha Takribani ya wanawake asilimia 36 Duniani, ni wataalamu wa sayansi, Tanzania tunalenga kufikia angalau asilimia 51 ya ushiriki wa wanawake” alisema Mkenda.
Aidha, alieleza kuwa Serikali imeendelea kuongeza fursa za elimu, ikiwemo ufadhili wa masomo kupitia Samia Skolashipu, kwa lengo la kuhamasisha wanafunzi kusoma fani za Sayansi, TEHAMA, Uhandisi na Sayansi Asilia.
Maadhimisho ya Wanawake na Wasichana katika Sayansi kwa mwaka 2026 yamekwenda sambamba na uzinduzi wa Kampeni ya “Africa Educate Her nchini Tanzania, inayolenga kuongeza upatikanaji wa elimu kwa wasichana na kuwapa fursa sawa za kujifunza na kufanikiwa.

.




