Na OWM – TAMISEMI, Colombia

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu -TAMISEMI Mhe. Prof. Riziki Shemdoe, ameongoza ujumbe wa Tanzania katika Mkutano wa Pili wa Kimataifa wa wa nchi zinazoshughulika na masuala Kilimo, Ardhi na Maendeleo vijijini, ulioanza Februari 24, 2026 nchini Colombia kwenye jiji la Cartegina.

Prof. Shemdoe amemuwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan katika mkutano huo, baada ya Mhe. Rais kupokea mwaliko wa kuudhuria mkutano huo kutoka kwa Rais Gustavo Petro Urrego wa Colombia.

Lengo kuu la mkutano huo uliohudhuriwa na nchi zaidi 100 duniani, ni kutoka na mwafaka wa namna gani matumizi bora ya ardhi katika kilimo yanaweza kupunguza migogoro ya ardhi na kuharakisha maendeleo vijijini.

Aidha nchi hizo zaidi ya 100 zilizoshiriki mkutano huo, ambazo zinashughulika na masuala ya Kilimo, Ardhi na Maendeleo ya Vijijini, zimepata fursa ya kubadilishana uzoefu katika masuala ya kilimo, Ardhi na Maendeleo Vijijini pamoja na matumizi ya teknolojia katika shughuli hizo, ambapo wananchi katika mataifa hayo watanufaika.

Katika Mkutano huo wa siku tano unaotarajiwa kufikia tamati Februari 28, 2026 Prof. Shemdoe ameambatana na Naibu Waziri wa Kilimo Mhe. David Silinde, wataalam kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu TAMISEMI na Wizara ya Kilimo, lengo likiwa ni kutimiza ndoto za Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan za kuleta mapinduzi ya kilimo nchini ili kuwanufaisha watanzania na kuwapatia tabasamu la kudumu.