Na OWM – TAMISEMI, Muheza

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu -TAMISEMI Mhe. Prof. Riziki Shemdoe, amewaelekeza Makatibu Tawala wa Mikoa na Wakurugenzi wa Halmashauri kutowahamisha au kuwaombea uhamisho watumishi wanaobainika kuwa na changamoto za kinidhamu katika Mamlaka za Mikoa na Serikali za Mitaa, na badala yake kuchukua hatua kwa kuwafungulia mashauri ya kinidhamu.

Prof. Shemdoe ametoa maelekezo hayo hivi karibuni akiwa katika kikao kazi na watumishi wa Muheza kilicholenga kuhimiza uwajibikaji katika usimamizi na matumizi ya fedha za miradi ya maendeleo, ikiwa ni utekelezaji wa maelekezo ya Waziri Mkuu Dkt. Mwigulu Nchemba, ambaye wakati wa ziara yake wilayani Muheza alibaini ubadhirifu wa fedha katika Mradi wa Jengo la Utawala na kumuelekeza Prof. Shemdoe na Waziri wa Ofisi ya Rais UTUMISHI na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete kuchukua hatua.

Aidha, Prof. Shemdoe amewaeleleza viongozi hao, kutotumia fedha au vifungu vya bajeti ya maendeleo kufanya malipo ya stahiki za watumishi, na kwamba fedha za mapato ya ndani zinazotengwa na Halmashauri kwa ajili ya miradi ya maendeleo zitumike kwenye shughuli zilizopangwa na si vinginevyo.

Sanjali na hayo, Prof. Shemdoe amewataka Wakurugenzi wa Halmashauri kuendelea kusimamia kikamilifu upatikanaji wa rasilimali fedha na matumizi sahihi ya rasilimali hizo ili kuwaletea wananchi maendeleo endelevu na tabasamu la kudumu.

Vivile, amewataka Makatibu Tawala wa Mikoa kufanya uchambuzi wa matumizi wa fedha za miradi ya maendeleo, pamoja na zinazotoka Serikali kuu na za mapato ya ndani katika kipindi cha kuanzia mwaka wa fedha 2024/25 hadi sasa, “Kama ikibainika kuna Halmashauri yoyote ina ubadhilifu na kuna watuhumiwa wa ubadhirifu huo mimi na Mhe. Ridhiwani Kikwete tutachukua hatua,” amesisitiza Prof. Shemdoe.

Hatua hiyo ya Prof. Shemdoe ni sehemu ya jitihada za kuunga mkono kwa vitendo azma ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kutaka fedha za miradi ya maendeleo kutumika katika kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi kupitia ujenzi wa miundombinu bora afya, elimu na barabara.