Na Mwandishi Wetu
MWANZILISHI Mtandao wa Afya na Elimu Kairuki (KHEN) na Hospitali ya Kairuki, Profesa Hubert Kairuki ametajwa kama mtu alieacha alama isiyofutika kwenye maisha ya watanzania kutokana na maono aliyokuwa nayo wakati wa uhai wake.
Hayo yaliibuliwa na washiriki wa mjadala wa kumbukumbu ya miaka 27 ya kifo cha Profesa Kairuki uliofanyika katika hospitali ya Kairuki Mikocheni jijini Dar es Salaam.

Watoa mada kwenye kongamano hilo walieleza namna walivyomfahamu Profesa Kairuki na namna alivyosimamia maono yake ya kuhakikisha anasaidi jitihada za serikali katika kutoa huduma za afya.
Mgeni rasmi kwenye kongamano hilo, Dk Egina Makwabe ambaye ni Mwenyekiti wa Chama cha Wenye Hospitali Binafsi (APHFTA), alisema Profesa Kairuki atakumbukwa kwa kuwa mstari wa mbele kuanzisha hospitali binafsi ya kwanza.
Alisema wakati huo ambapo serikali haikuwa inaruhusu watu binafsi kuwa na hospitali, Profesa Kairuki alisimama kidete kuhakikisha anatimiza ndoto zake na alifanikiwa kuanzisha hospitali hiyo akiwa miongoni mwa watu wachache kabisa wa mwanzo.
Dk Makwabe alisema mbali na kuanzisha hospitali hiyo pia alipambana kuhakikisha wenye hospitali binafsi wanakuwa na sauti moja yenye nguvu kuwasilisha madai yao serikali.
“Alikuwa na maono makubwa sana na ya muda mrefu, aliwaambia wenzake kuwa tukiwa mmoja mmoja maoni yetu yatapuuzwa kwa hiyo tupambane tuwe na sauti moja na alifanikiwa kuanzisha hii APHFTA mnayoiona leo ni maono na jitihada zake,” alisema.

Aidha, Dk Makwabe alisema anajivunia kuwa mmoja wa watu waliowahi kufanyakazi kwenye taasisi iliyoanzishwa na Profesa Kairuki kwani alipofanyakazi hapo alijiona yuko sehemu salama.
“Nilitamani sana siku moja nije kuwa kama Profesa Kairuki kutokana na uchapakazi wake na maono yake ya muda mrefu, nimejitahidi kutaka kuwa kama yeye lakini bado nina safari ndefu,” alisema Dk Makwabe.
Mwenyekiti wa KHEN, Kokushubira Kairuki alisema Profesa Kairuki alimuwa mtu wa kujituma na kutumia muda wake mwingi kufanya kazi kufanikisha yale anayoamini.
“Muda mwingi alipenda kufanyakazi wakati mwingine alikuwa anakuja anakuta tumeshalala, alipenda kuona mambo makubwa yanafanyika kwenye sekta ya afya, alikuwa na maono ya muda mrefu sana ambayo sisi tuliobaki tutajitahidi kuyasimamia yatokee,” alisema
Makamu Mkuu wa Chuo cha Kairuki, Profesa Yohana Mashalla, alisema anajisikia fahari kuwa mmoja wa watu waliofundishwa udaktari na Profesa Kairuki kutokana na umahiri na upendo aliokuwa nao kwenye fani yake.

“Kuna wakati alitupeleka kwenye mafunzo ya vitendo Mtwara, tulienda kwa njia ya meli sasa tulipofika Kilwa Masoko wenzangu wakashuka kwenda kuzunguka nje, meli ilipokaribia kuondoka akaniambia kawaite wenzako wasije wakaachwa hapa,” alisema
“Nilikwenda kuwatafuta ingawa sikujua wako wapi nilizuzunguka sana na muda ule nawapata tunarudi tukakuta meli imeshaondoka, tulikaa pale siku mbili ndipo tukapata usafiri wa kwenda Mtwara kwa barabara,” alisema
“Tulipofika Mtwara tulijua cha moto tutakiona lakini cha kushangaza Profesa Kairuki alitupokea kwa upendo sana akasema karibuni wana wapotevu. Kila mmoja wetu alishangaa kwasababu tulitarajia kukaripiwa sana,” alisema na kuongeza
“Na cha kushangaza zaidi tulipomaliza mafunzo yetu kwa vitendo alitutafutia usafiri wa ndege kwa mara ya kwanza tukapanda ndege tukarudi Dar es Salaam, kwa hiyo ni mtu aliyekuwa na upendo sana na watu wote kwenye jamii,” alisema





