Dkt. Biteko azindua Kitabu cha Living with Cancer cha Prof. Mark Mwandosya
Watanzania watakiwa kujenga utamaduni wa kupima afya
Serikali yaimarisha huduma za uchunguzi na matibabu ya saratani
Na Ofisi ya Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amemuelezea Prof. Mark Mwandosya kuwa ni Shujaa wa Saratani ya Damu (Multiple Myeloma) ambaye ameishi na Saratani kwa zaidi ya miaka 14.
Dkt. Biteko amesema hayo (Julai 29) jijini Dar es Salaam katika uzinduzi wa kitabu cha Maisha ya Mgonjwa anayeishi na Saratani ya Damu Multiple Myeloma (Living with Cancer: Diaries of Multiple Myeloma Patient) kilichoandikwa na Prof. Mark Mwandosya ambaye ni msomi, mwandishi na mwanasiasa wa muda mrefu nchini.
“Katika miaka 14 ya kishujaa, Prof. Mwandosya amekuwa shuhuda kwetu sote kuwa endapo utafuata hatua stahiki za matibabu, unaweza kupona saratani na kuendelea kuishi maisha bora. Asante sana na hongera sana Profesa. Mwenyezi Mungu azidi kukubariki,” Amesema Dkt. Biteko.

Amesema kupitia historia ya Prof. Mwandosya ya matibabu yake ya saratani Kitabu hicho kitasaidia kunusuru maisha ya watanzania wengi ambao wangeweza kushindwa kunufaika na huduma za matibabu kwa kukosa taarifa sahihi.
“Nakupongeza sana tena Profesa kwa kujitoa kuwa sehemu ya ushuhuda ili watanzania na Dunia ijifunze kupitia maisha yako.Hakika huu ni upendo wa hali ya juu kwa nchi yako. Nami kwa niaba ya Serikali nakupongeza kwa uamuzi wako huu. Aidha, ninakuombea kwa Mungu akupe afya njema na maisha marefu zaidi na zaidi, ” Amesema Dkt. Biteko.
Amesema kuwa, saratani ni ugonjwa ambao unaweza kudhibitiwa au kutibiwa na kupona kabisa endapo mgonjwa atapata matibabu kwa wakati na kumshukuri Profesa Mwandosya kwa kuamua kuwa miongoni mwa watu wanaoleta suluhisho la tatizo hili kwa jamii.
Kwa upande wake, Prof. Mwandosya amesimulia safari yake ya kuishi na ugonjwa wa Multiple Myeloma, aina adimu ya saratani ya damu inayodumu kwa muda mrefu. Amesema kupitia ugonjwa huo ameamua kueleza changamoto na mafunzo ya kimwili, kiakili na kiroho aliyopitia akisisitiza ujumbe wa matumaini, ujasiri na heshima katika maisha.
“Ugunduzi wa Saratani haupaswi kuchukuliwa kama hukumu ya kifo ni safari ya kuendelea kuishi na kutafuta maana na nguvu hata katikati ya maradhi, amesema Prof. Mwandosya.

Naye, Mtaalamu wa magonjwa ya damu na mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS), Dkt. Clara Chamba ametoa rai kwa watanzania kufanya uchunguzi wa afya mapema na kupenda kufanya mazoezi
Katika kupambana na Saratani, Serikali kupitia Wizara ya Afya imefanya uwekezaji mkubwa katika huduma za uchunguzi na matibabu ya saratani na magonjwa mengine kwa ujumla.

