Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam
Wizara ya Madini imekamilisha maandalizi ya program ya MBT ambayo itatekelezwa katika kipindi cha miaka mitano kuanzia mwaka 2025 hadi 2030.
Waziri wa Madini, Anthony Mavunde amesema kuwa Programu hii ni ya kimageuzi katika Sekta ya Madini ambayo imeanzishwa kwa ajili ya kushughulikia changamoto na kuboresha fursa kwa wanawake, vijana na watu wenye mahitaji maalum ili kuongeza ushiriki wa makundi hayo katika mnyororo wa thamani wa madini.
Amesema Programu hii inatarajiwa kuwa na matokeo kama kuongeza kipato na kuboresha maisha ya wanawake, vijana na wenye mahitaji maalum; kuwaongezea fursa za ajira; na kuongezeka kwa kiwango cha uwekezaji kwa wanawake, vijana na watu wenye mahitaji maalum katika Sekta ya Madini.
“Aidha, Programu hii itasaidia kuboresha viwango vya afya, usalama na utunzaji wa mazingira katika maeneo yenye shughuli za madini, ” amesema.

UNUNUZI WA DHAHABU KUPITIA BENKI KUU YA TANZANIA
Mavunde amesema kuwa Machi 2024, aliunda Kamati ya Wataalam kwa ajili ya kufanya majadiliano na wamiliki wa leseni za uchimbaji madini ya dhahabu nchini, ikiwa ni utekelezaji wa Kifungu cha 59 cha Sheria ya Madini Sura 123.
“Kifungu hicho kilikuwa kinamuelekeza Waziri kufanya majadiliano na wamiliki wa leseni za uchimbaji madini ya dhahabu, ili watenge sehemu ya uzalishaji wa madini yao kwa ajili ya kuchenjuliwa, kuyeyushwa au kusafishwa hapa nchini. Baada ya kuanza majadiliano, Kamati ilibaini mapungufu katika Kifungu cha 59 cha Sheria ya Madini, Sura ya 123, kwa kuwa kilikuwa kinawapa wazalishaji wa dhahabu uhuru wa kuchagua hatua ya uchakataji badala ya kuwataka kutekeleza hatua zote.
“Kamati ilipendekeza yafanyike maboresho ya sheria mbalimbali ili kuwezesha: kwanza kuendeleza viwanda vya uchakataji, uchenjuaji, na usafishaji wa madini ya dhahabu nchini.
“Pili Benki Kuu ya Tanzania kununua dhahabu inayozalishwa nchini ili kukuza hifadhi ya fedha za kigeni kupitia “monetary gold” ambayo ina manufaa makubwa kwa ukuaji na ustahimilivu wa Uchumi wa Taifa kwa kuwa nchi yetu, pamoja na mambo mengine, inaagiza bidhaa nyingi kutoka nje ambazo zinahitaji kulipiwa kwa fedha za kigeni.

“Tatu kuruhusu sehemu ya dhahabu inayozalizwa hapa nchini kufanyiwa biashara ndani ya masoko yaliyopo nchini ili kuchangamsha uchumi na kuwawezesha wadau wengine wanaohitaji dhahabu kama vile masonara na viwanda vya kusafisha dhahabu kupata dhahabu hapa hapa nchini.
“Kufuatia maboresho ya kifungu cha 59 cha Sheria ya Madini, Sura ya 123, Serikali kupitia Benki Kuu ya Tanzania (BoT) ilianza rasmi ununuzi wa dhahabu tarehe 1 Oktoba 2024, kupitia viwanda vitatu vya kusafisha dhahabu vya MPMR (Mwanza), GGR (Geita), na Eyes of Africa (Dodoma). Hadi kufikia tarehe 31 Machi 2025, jumla ya Kilo 3,061 sawa na tani 3.061 za dhahabu zilinunuliwa na BoT kwa gharama ya Shilingi bilioni 702.3. Kati ya kiasi kilichonunuliwa takribani, Kilo 2,954 zilisafishwa katika viwanda vya kusafisha dhahabu vilivyoko nchini” amesema Mavunde.
KUWAENDELEZA WACHIMBAJI WADOGO
Amesema kuwa Serikali inatambua na kuthamini mchango wa shughuli za uchimbaji mdogo nchini katika kutoa ajira, kuboresha kipato cha mtu mmoja mmoja na kukuza uchumi wa nchi kwa ujumla. Kwa kutambua hilo, Serikali ya Awamu ya Sita imekuwa ikifanya juhudi mbalimbali za kuboresha shughuli za uchimbaji mdogo nchini.

Amesema kuwa Serikali kupitia Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) imefanikiwa kununua mitambo 15 ya uchorongaji miamba kwa ajili ya kutoa huduma kwa wachimbaji wadogo.
Amesema kuwa kufuatia ununuzi wa mitambo hiyo, STAMICO imeendelea kutoa huduma ya uchorongaji kwa bei nafuu kwa wachimbaji wadogo. Aidha, katika kipindi husika wachimbaji wadogo 16 tayari wamepata huduma hiyo katika maeneo ya Tambi – Mpwapwa, Nyawa – Bariadi, Matondo, Makongolosi na Matundasi – Chunya, Lwamgasa, Nyaruyeye, Nyamalimbe na Nyakagwe – Geita, Mavota – Biharamulo, Endabash – Karatu, Mwakitolyo – Shinyanga na Mbangala – Songwe.
Amesema kuwa katika utekelezaji huo, jumla ya mita 3,450.37 zimechorongwa katika maeneo hayo. Wizara kupitia Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) imeendelea kuratibu shughuli za uchimbaji mdogo kwa kutoa huduma za kitaalamu kwa wachimbaji wadogo katika nyanja za utafiti, uchimbaji, uchenjuaji madini pamoja na utunzaji wa mazingira.
Jumla ya wachimbaji wadogo 471 wamepatiwa mafunzo kupitia vituo vya mfano vya Katente, Lwamgasa na Itumbi ambapo mpaka sasa wachimbaji 12 wa madini wameanzisha vituo vyao baada ya kujifunza kupitia vituo hivyo.

Aidha, kupitia vituo hivyo vya mfano, huduma ya uchenjuaji mbale za dhahabu kwa wateja 41 ilitolewa ambapo dhahabu ya uzito wa kilogramu 119.57 yenye thamani ya Shilingi 23,318,849,170.45 ilichenjuliwa.
Amesema kuwa Wizara kupitia Tume ya Madini imeendelea kutenga maeneo mahsusi kwa ajili ya wachimbaji wadogo ambapo hadi kufikia Machi 2025 maeneo 58 yametengwa katika mikoa ya kimadini ya Geita, Mara, Mbogwe, Kahama, Chunya na Songwe.
UONGEZAJI THAMANI MADINI
Ili kuimarisha shughuli za uongezaji thamani madini nchini. Wizara imeanza ujenzi wa jengo la ghorofa nane (8) katika Kituo cha Jemolojia Tanzania (TGC) kwa ajili ya shughuli za kituo hicho. Jengo hilo litakuwa na miundombinu ya madarasa, mabweni ya wanafunzi, karakana za uongezaji thamani madini, maabara za madini ya vito, duka la bidhaa za usonara, ofisi na kantini;

Utoaji wa Leseni za uendeshaji wa shughuli za Madini
Amesema kuwa Serikali ya Awamu ya Sita kupitia Tume ya Madini imekuwa ikitoa leseni za uendeshaji wa shughuli za madini kwa wadau wake kwa kuzingatia Sheria ya Madini, Sura 123. Katika kipindi cha kuanzia 2021/2022 hadi Mei, 2025 Tume ya Madini imetoa jumla ya leseni 34,348 ikijumuisha leseni za Uchimbaji Mkubwa, Uchimbaji wa Kati, Uchimbaji Mdogo, biashara ya madini pamoja na uchenjuaji wa madini.
“Mathaani katika kipindi hicho, Tume ya Madini imetoa leseni kubwa za uchimbaji wa madini kwa kampuni mbalimbali za uchimbaji wa madini ikiwemo kampuni ya Faru Graphite Corporation Limited itakayojihusisha na uchimbaji wa madini ya kinywe Wilayani Mahenge; Mamba Minerals Corporation Limited inayojihusisha na uchimbaji wa Rare Earth Elements-REE katika eneo la Ngualla yenye iliyopo mkoani Songwe; Sotta Mining Corporation Limited iliyopo Mkoani Mwanza, Wilaya ya Sengerema; Leseni ya usafishaji madini kwa kampuni ya Tembo Nickel Refining Company Limited iliyopo katika Wilaya ya Ngara Mkoani Kagera; na Leseni ya uchimbaji wa madini ya kinywe kwa Kampuni ya Duma Tanzgraphite Limited (DTL) katika eneo la Epanko, Wilaya ya Ulanga” amesema.
Amesema kuwa utafiti kwa kutumia Teknolojia ya Kisasa; Wizara inaendelea na maandalizi ya kufanya utafiti kwa kutumia teknolojia ya kisasa ya kurusha ndege “High Resolution Geophysical Survey” ili kuongeza eneo lenye taarifa za kina za jiofizikia kutoka asilimia 16 za sasa hadi kufikia asilimia 34 ifikapo mwaka 2026.
MIPANGO INAYOTARAJIWA KUTEKELEZWA
Waziri Mavunde amesema uwa pamoja na mafanikio ya sekta ya madini niliyoyataja, Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, inaendelea kubuni mipango mbalimbali ambayo itawezesha sekta ya madini kuendelea kutoa mchango mkubwa katika ukuaji wa uchumi wa nchi.

Miongoni mwa mipango ambayo ipo mbioni kutekelezwa ni pamoja na Kuimarisha Mpango wa Ununuzi wa Dhahabu kupitia Benki Kuu ya Tanzania; Maboresho yafuatayo yanatarajiwa katika Mpango wa ununuzi wa dhahabu wa Benki Kuu ili kufikia malengo kusudiwa ya Serikali ya kuwa na ununuzi wa dhahabu endelevu na wenye tija: –
Kwanza Serikali kupitia Benki Kuu ya Tanzania itaandaa mwongozo utakaotumika kuwatambua, kuwatathmini na kuwachagua wauzaji wa dhahabu (Due diligence and Know Your Customer – KYC). Mwongozo utabainisha sifa na vigezo vya kuiuzia Benki Kuu dhahabu kutoka kwa wachimbaji na wafanyabiashara. Aidha, mwongozo huo utabainisha sifa na vigezo vitakazozingatiwa wakati wa kuteua viwanda vya kusafisha dhahabu ya Benki Kuu;
Pili kwa kuwa si kila dhahabu itakayonunuliwa na Benki Kuu ya Tanzania itakuwa na sifa za kuingia kwenye soko la LBMA ili kuhifadhiwa kama dhahabu fedha (Monetary gold), Benki Kuu itatakiwa kuwa na mifumo miwili ya ununuzi; Mfumo wa kwanza utakuwa ni kwa ajili ya dhahabu inayotokana na migodi mikubwa, wachimbaji wadogo na wakati inayokidhi vigezo vya LBMA. Mfumo wa pili utakuwa kwa ajili ya kununua dhahabu ya wachimbaji wadogo na wafanyabiashara wakubwa (Dealers) ambayo haitafikia vigezo vya LBMA;
Tatu pia, Serikali kupitia Benki Kuu, inaangalia uwezekano wa kuanzisha uuzaji wa sarafu za dhahabu zenye uzito wa 1 oz, ½ oz, na ¼ oz ili kuwaongezea watanzania wigo wa uwekaji akiba na uwekezaji kupitia ununuzi wa dhahabu. Vilevile hatua hii itaongeza umiliki wa dhahabu miongoni mwa wananchi, kuimarisha soko la ndani la dhahabu, na kuimarisha mzunguko wa fedha ndani ya nchi.
UNUNUZI WA MAFUTA NA FEDHA ZA KIGENI KUTUMIA DHAHABU
Vilevile, Serikali kupitia Benki Kuu, itafikiria kuanzisha utaratibu wa kutumia dhahabu itakayonunuliwa, hususan isiyokidhi vigezo vya kuingia katika soko la LBMA, kubadilishana na nishati ya mafuta (barter trade) na kununulia fedha za kigeni kulingana na mahitaji ya nchi.
Sheria inayotaka kampuni na wafanyabiashara kurejesha fedha zinazotokana na mauzo ya bidhaa nje ya nchi, ikiwemo madini, itaendelea kusimamiwa ipasavyo. Iwapo Serikali itaipa Benki Kuu ya Tanzania haki ya kwanza (Pre-emption right) ya kununua fedha hizo zinazorejeshwa nchini na kuwalipa wahusika kwa Shilingi ya Tanzania itasaidia upatikanaji wa fedha za kigeni na kuimarisha umadhubuti wa shilingi na viwango vya ubadilishaji fedha.
Sekta ya Madini ni miongoni mwa sekta muhimu katika kukuza uchumi na kuleta maendeleo ya kijamii na Taifa kwa ujumla. Mafanikio makubwa yaliyopatikana katika kipindi cha Serikali ya Awamu ya Sita katika sekta hii yametokana na uongozi makini wa Rais Samia Suluhu Hassan. Aidha ukuaji katika sekta hii umesaidia kuongeza mapato ya Serikali na kukua kwa Mchango wa Sekta ya Madini nchini.