Na Tatu Mohamed, JamhuriMedia, Dar es Salaam

BODI ya Wataalam wa Ununuzi na Ugavi (PSPTB) imetangaza kuendesha Mitihani ya 31 ya kitaaluma kuanzia tarehe 25 hadi 29 Agosti, 2025, jijini Dodoma, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuimarisha taaluma na uwajibikaji katika sekta ya ununuzi na ugavi nchini.

Akizungumza Julai 4, 2025, wakati wa Maonesho ya 49 ya Biashara ya Kimataifa (Sabasaba), Mkurugenzi Mtendaji wa PSPTB, Godfred Mbanyi, alieleza kuwa usajili wa mitihani hiyo tayari umefunguliwa rasmi kupitia tovuti ya bodi hiyo (https://registration.psptb.go.tz) na utahitimishwa tarehe 15 Agosti, 2025.

“Tunawaalika waombaji wote wenye sifa kujiandikisha mapema na kujiandaa kupitia madarasa ya maandalizi. Mitihani hii ni muhimu kwa kukuza taaluma na kuongeza ufanisi katika utendaji wa sekta ya ununuzi,” alisema Mbanyi.

Amefafanua kuwa waombaji wanaostahili ni pamoja na wahitimu wa fani ya ununuzi na ugavi kwa ngazi zote (Astashahada, Stashahada, Shahada), wafanyakazi wa umma na binafsi wanaotekeleza majukumu ya ununuzi bila vyeti rasmi vya kitaaluma, pamoja na waliowahi kufanya mitihani ya PSPTB awali na wanarudia au wanaendelea na ngazi zinazofuata.

Mbanyi alieleza kuwa watahiniwa wanaorudia mitihani zaidi ya ngazi moja wanaruhusiwa kuunganisha ngazi mbili zinazofuatana (Two Consecutive Blocs), kwa idadi ya masomo kati ya mawili hadi sita, kulingana na ratiba rasmi ya Mitihani ya 31.

Kuhusu ada, PSPTB imetoa maelezo kwenye tovuti yao rasmi, huku ikihimiza waombaji kutembelea ukurasa huo kwa taarifa zaidi.

Mbanyi alisisitiza kuwa mitihani mingine ya kawaida inayofanyika mwezi Mei na Novemba itaendelea kama kawaida kwa mujibu wa ratiba ya bodi hiyo.

“Lengo letu ni kuhakikisha sekta ya ununuzi na ugavi inakuwa na wataalam wenye viwango, wanaotambulika kisheria na kitaaluma. Hili ni eneo nyeti katika matumizi ya rasilimali za umma na tija ya taifa kwa ujumla,” alihitimisha.