Na Tatu Mohamed, JamhuriMedia, Dar es Salaam
MAMLAKA ya Kudhibiti Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA) imesema inajivunia utekelezaji wa agenda ya Nishati Safi ya kupikia iliyoasisiwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuwa imeanza kutekelezwa kwa vitendo na kuonyesha mafanikio makubwa.
Akizungumza katika Maonesho ya 49 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam maarufu kama Sabasaba, Mkurugenzi Mkuu wa PURA, Charles Sangweni, amesema mwitikio wa wananchi kuhusu nishati safi umekuwa mkubwa, na kwamba mamlaka hiyo imejipanga kuhakikisha haina mwanya wa kumuangusha Rais katika agenda hiyo muhimu ya kitaifa.

“Katika maonesho haya ya Sabasaba, tumeona mwamko mkubwa wa wananchi katika masuala ya nishati safi ya kupikia. Hii inaonyesha uelewa unaongezeka, na sisi kama PURA tunaitekeleza agenda hii kikamilifu,” amesema Sangweni.
Ameeleza kuwa PURA imekuwa mshiriki wa kudumu wa maonesho hayo tangu mwaka 2017, na kwamba kila mwaka kumekuwa na maboresho ya kimkakati katika ushiriki wao. Kwa mwaka huu, amesema, mambo yameimarika zaidi, hasa kwenye matumizi ya mifumo ya kidijitali na ongezeko la idadi ya wananchi wanaotembelea banda lao.
“Watu wanauliza maswali ya msingi, yenye maana na yanayoonyesha namna uelewa kuhusu sekta ya mafuta na gesi ulivyopanuka. Tunapokea maoni, changamoto na maulizo ambayo yanatusaidia pia kuboresha utendaji wetu,” amesema.
Akizungumzia nafasi ya Watanzania katika sekta ya mafuta na gesi, Sangweni amesema tangu kuanzishwa kwa PURA, kumekuwa na ongezeko kubwa la ushiriki wa Watanzania, ambapo kwa sasa asilimia 85 ya ajira katika sekta hiyo zinashikiliwa na wazawa, ikilinganishwa na chini ya asilimia 55 hapo awali.
“Uzoefu na uelewa vimeongezeka. Awali meli zilikuja na wafanyakazi kutoka nje pekee, lakini sasa hata Watanzania wapo ndani ya timu hizo. Hili ni jambo la kujivunia,” amesema.

Kwa mujibu wa Sangweni, PURA kwa sasa iko kwenye maandalizi ya kuchimba visima vitatu katika eneo la Mtwara, huku ushiriki wa Watanzania katika vitalu hivyo ukiwa umefikia asilimia 40. Pia amesema kati ya kampuni 10 zinazofanya utafiti wa mafuta na gesi nchini, sita zinamilikiwa na Watanzania.
“Kwenye nafasi za uongozi ndani ya sekta, karibu asilimia 95 zinashikiliwa na Watanzania. Hii inadhihirisha dhamira ya Serikali ya kuhakikisha rasilimali zetu zinawanufaisha wananchi,” amesema.
Amehitimisha kwa kuipongeza Serikali kwa kuweka mazingira rafiki ya uwekezaji na ushirikishwaji wa Watanzania katika miradi ya kimkakati, akisisitiza kuwa PURA itaendelea kuhakikisha kila hatua ya maendeleo inawagusa Watanzania moja kwa moja.
