Na Mwamvua Mwinyi, JamhuriMedia, Rufiji
MKOA wa Pwani una zaidi ya ranchi ndogo 800, mfumo unaowawezesha wafugaji kumiliki maeneo rasmi ya malisho, kutambua mifugo yao pamoja na kupunguza migogoro kati ya wakulima na wafugaji.
Mpango huo ulizinduliwa Novemba 2024 mkoani humo kwa kugawa hati za kimila, ambapo utekelezaji wake ulianza katika vijiji 15 kupitia wilaya za Rufiji, Mkuranga, Kibiti na Kisarawe.
Akizungumza katika ranchi ndogo ya Chumbi C, wilayani Rufiji, wakati akizungumza na mfugaji Lisesi Kundugu, Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Abubakar Kunenge, alisema wafugaji wanapaswa kufuga kwa njia za kisasa huku wakulima wakilima kwa tija, akibainisha kuwa mkoa una mipango madhubuti ya matumizi bora ya ardhi.
Kunenge alieleza, Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan anatamani kuona wafugaji na wakulima wakifanya shughuli zao kwa njia za kisasa, kitaalamu na kwa tija ili kuinua maisha yao kiuchumi.
“Ardhi haiongezeki, watu wanaongezeka na shughuli za kiuchumi zinaongezeka, “Hivyo, ardhi kidogo tuliyonayo itumike kwa utaalamu ili kuleta manufaa ya kiuchumi,” alisisitiza Kunenge.
Aidha, Kunenge alimpongeza Mkuu wa Wilaya ya Rufiji, Luteni Kanali Fredrick Komba, kwa mipango na usimamizi mzuri uliosaidia kudhibiti migogoro kati ya wakulima na wafugaji wilayani humo.
Kwa upande wake, Komba alielezea kwamba, wilaya hiyo imekuwa na mkakati wa kuanzisha ranchi ndogo tangu mwaka 2023 sanjali na kutoa elimu kwa wafugaji.
“Mpaka Oktoba 2025 tulikubaliana na wafugaji kwamba ifikapo Januari 2026 wote wawe wamehamia kwenye ranchi ndogo ili kuwezesha kupata idadi halisi ya mifugo, na itakayobaki nje itachukuliwa hatua,” alibainisha Komba.
Vilevile, Komba alisema kuanzia Februari mwaka huu wilaya hiyo itaanza usajili mpya wa wafugaji, ambapo taarifa zitakazokusanywa zitahusisha jina la mfugaji, namba ya kitalu na idadi ya mifugo.
Naye mfugaji Lisesi Kundugu aliipongeza Serikali kwa mipango ya matumizi bora ya ardhi, akisema hatua hiyo imepunguza ufugaji holela na changamoto za upatikanaji wa malisho na maji.
“Kwangu mimi, ranchi ndogo imekuwa mkombozi, Changamoto za malisho na maji zimepungua, nafuga kisasa na naamini ufugaji wangu wa kitaalamu utakuwa mfano kwa wengine,” alieleza Lisesi.






