Na Mwamvua Mwinyi, JamhuriMedia, Pwani

MKUU wa Mkoa wa Pwani, Abubakar Kunenge, amesema mkoa huo unaendelea kutekeleza vipaumbele vya Serikali kwa vitendo, hususan katika eneo la uzalishaji wa ajira kwa vijana, hatua inayolenga kumuunga mkono Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Kunenge alitoa kauli hiyo wakati wa ziara yake ya kutembelea kongani ya viwanda ya Gaini Company Limited iliyopo Kata ya Kikongo, wilayani Kibaha mkoani Pwani, ambapo mradi huo unatarajiwa kuzalisha ajira zipatazo 1,500 ifikapo Machi 2026.

Alisema uwekezaji huo unaendana kikamilifu na mkakati wa Serikali wa kukuza uchumi wa viwanda na kuongeza fursa za ajira kwa wananchi, hususan vijana, jambo linalochochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii .

Alieleza Mkoa wa Pwani unaendelea kushirikiana kwa karibu na taasisi wezeshi zikiwemo TANESCO, DAWASA na TANROADS, ili kuhakikisha mazingira ya uwekezaji yanakuwa rafiki na yasiyo na urasimu. 

Aidha, Kunenge alisema mradi wa bomba la gesi kutoka Kinyerezi hadi Chalinze tayari umefanyiwa upembuzi yakinifu wenye thamani ya shilingi bilioni 2.3 na Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), hatua itakayoongeza ufanisi wa upatikanaji wa nishati kwa viwanda mkoani Pwani.

Kwa upande wake, Meneja wa Mradi wa kongani hiyo, QS Bradley Cuthbert Muro, amesema ujenzi wa viwanda viwili umefikia hatua za mwisho, kiwanda cha chuma kimefikia asilimia 85 ya ujenzi huku kiwanda cha cubes kikifikia asilimia 95 na uzalishaji katika viwanda hivyo unatarajiwa kuanza Machi mwaka huu.

Kongani hiyo itajumuisha viwanda vya aina mbalimbali vikiwemo heavy duty industries, medium industries na light duty industries, ikiwemo viwanda vya uzalishaji wa nondo, mabati, mabomba ya chuma (steel pipes), hollow sections za aina ya RHS, SHS na CHS, flat bars pamoja na misumari.