Na Mwamvua Mwinyi, JamhiriMedia, Pwani

Jumla ya vituo 3,941 vya kupigia kura vimeandaliwa katika Mkoa wa Pwani kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Oktoba 29, 2025, kwa mujibu wa Mratibu wa Uchaguzi wa mkoa huo, Gerald Mbosoli.

Mbosoli amesema kuwa jumla ya wananchi zaidi ya milioni 1.413 wenye sifa wanatarajiwa kushiriki katika zoezi la kupiga kura mkoani humo, huku maandalizi yakiwa katika hatua za mwisho.

Vituo hivyo vitakuwa wazi kuanzia saa 1:00 asubuhi hadi saa 10:00 jioni, na kuwa Tume imezingatia mahitaji ya makundi maalum ikiwemo wazee, wajawazito na watu wenye ulemavu, kwa kuhakikisha wanapata huduma kwa haraka na kwa mazingira rafiki.

Kwa mujibu wake, kampeni zitafungwa rasmi Oktoba 28, siku moja kabla ya uchaguzi.

Mbosoli ametoa wito kwa wananchi wote wa Mkoa wa Pwani kujitokeza kwa wingi kupiga kura kwa amani, akisisitiza kuwa ni haki ya msingi ya kila Mtanzania.