Na Mwamvua Mwinyi,JamhuriMedia, Pwani
SERIKALI kupitia Bodi ya Korosho imetoa jumla ya miche ya korosho milioni 4.2 nchini, ambapo kati ya miche hiyo, mkoa wa Pwani umepatiwa miche milioni 1.5, sawa na asilimia 35.7 ya miche iliyotolewa.
Akizungumza na wakazi wa Chumbi A wilayani Rufiji, wakati mkoa huo ulipoungana na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika zoezi la upandaji miti na ugawaji wa miche milioni 1.5, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya siku yake ya kuzaliwa Januari 27,2026, Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Abubakar Kunenge, aliwataka wananchi kuitumia miche hiyo kama fursa ya kujikomboa kiuchumi.

Alieleza katika msimu wa mwaka 2025/2026, mkoa wa Pwani ulizalisha tani 25,000 za korosho dhidi ya lengo la tani 30,000, huku matarajio yakiwa ni kufikia uzalishaji wa tani 73.4 ifikapo mwaka 2029/2030.
“Naona wivu kusikia Ruvuma kuzalisha tani 40,000, Tutumieni neema ya miche tuliyopata kuinua kilimo chetu pamoja na kutunza mazingira”
“Mheshimiwa Rais anafanya linalostahili kufanya awezalo, anatimiza wajibu wake katika kuinua sekta ya kilimo kwa kuleta pembejeo, miche bora, mbolea, sulphur ili kuboresha maisha ya wakulima” alieleza Kunenge.

Aliwataka wakulima wa korosho Rufiji kulima kilimo cha kisasa na kusafishia mashamba yao.
Vilevile Kunenge alifafanua, wilaya zote saba mkoani humo zimeendesha zoezi la upandaji wa miti 6,379, ikiwemo miti 671 ya matunda na miti 5,708 ya mbao na vivuli.
“Zoezi hili ni sehemu ya kuunga mkono juhudi na maono ya Serikali katika kulinda na kutunza mazingira, hususan katika kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.”
Akishiriki upandaji miti Mkuu wa wilaya ya Rufiji, Luteni Kanal Faustine Komba alisema mkoa umeipa heshima wilaya hiyo na kuweka historia katika kumbukizi ya siku ya kuzaliwa kwake Rais Samia.

Komba alibainisha wilaya inaendelea kuhimiza wananchi kulima mazao mbalimbali ikiwemo zao la kibiashara la korosho.
Ofisa Kilimo Halmashauri ya Rufiji,Ryoba Magabe alisema, hadi sasa kuna wakulima wa korosho 6,363 wenye mikorosho milioni 1.132 kwa mujibu wa takwimu za usajili wa wakulima wa zao hilo mwezi Mei mwaka 2025.
Alielezea kwamba, Halmashauri inatoa huduma ya wataalamu wa ugani kwa wakulima, inahamasisha kulima zao hilo ambapo shamba la Bodi ya korosho lina hekari 6,500 na shamba la Halmashauri hekari 3,500 na mashamba mapya ya wakulima.
Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan amedhimisha siku yake ya kuzaliwa Januari 27, 2026 kwa kuongoza zoezi la upandaji miti Kizimkazi, Zanzibar, akitimiza miaka 66 tangu kuzaliwa mwaka 1960 katika Kijiji cha Kizimkazi, Mkoa wa Kusini Unguja.




