Na Mwandishi Wetu,JamhuriMedia, Dar es Salaam

Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Kinondoni imefanikiwa kukamata raia wa China wakiwa na fedha haramu zaidi ya Shilingi bilioni mbili, katika operesheni maalum iliyohusisha vyombo mbalimbali vya uchunguzi.

Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam, Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Kinondoni, Christian Nyakizee, amesema operesheni hiyo ilianza Mei 2025 na kudumu kwa takribani miezi saba, ikihusisha TAKUKURU kwa kushirikiana na vyombo vingine vya uchunguzi, Benki Kuu ya Tanzania (BoT), mabenki ya biashara pamoja na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).

Amesema uchunguzi huo ulilenga uhalifu unaohusisha matumizi ya taarifa za kadi za benki zilizoibwa ili kujipatia fedha.

Kwa mujibu wa Nyakizee, watuhumiwa ni raia wa mataifa mbalimbali wakiwemo Wachina na Watanzania, huku waliodhurika wakiwa ni raia wa nchi tofauti nje ya Tanzania, ikiwemo Marekani, Canada, Colombia, Argentina, Japan, Uruguay, Denmark, Uholanzi, New Zealand, Australia na China

Ameeleza kuwa fedha huondolewa kwenye akaunti binafsi za waathirika, kisha kuonekana zimetumika kwa njia ya kadi kulipia huduma mbalimbali nchini Tanzania, ilhali wahusika hawajawahi kufika wala kupata huduma nchini humo katika kipindi husika.

Uchunguzi umebaini kuwa wahalifu hutumia njia za malipo za kielektroniki ikiwemo mashine za POS, payment links, miamala ya e-commerce pamoja na control numbers kulipia huduma za utalii, afya, malazi, usafiri wa anga pamoja na kodi mbalimbali za Serikali

Nyakizee amesema wanaohusishwa na wizi wa taarifa za kadi wanatoka katika nchi za Cameroon, Nigeria, Pakistan, Bulgaria, Macedonia, Poland, Romania na China, huku wakishirikiana na Watanzania katika kutoa fedha hizo

Ameongeza kuwa fedha hizo huingizwa katika akaunti za makampuni ya wafanyabiashara wengi wao wakiwa vijana wa Kitanzania wanaomiliki akaunti kwenye mabenki mbalimbali, kisha hutolewa taslimu na kugawanywa kwa makubaliano ya asilimia.

Hadi sasa, amesema watuhumiwa zaidi ya 137 wamekamatwa, kupekuliwa na kuhojiwa katika mikoa ya Arusha, Kilimanjaro, Mwanza, Dar es Salaam na Zanzibar. Uchunguzi wa awali umebaini kuwa zaidi ya Shilingi bilioni 18 zimetakatishwa kwa mtindo huo katika kipindi cha miaka minne kuanzia 2022 hadi 2025.

Amesema tayari mashauri matatu yamefunguliwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kwa makosa ya ukwepaji kodi, utakatishaji fedha na uhujumu uchumi, yenye namba ECC 21633/2025, ECC 29134/2025 na ECC 29143/2025.

Kati ya waliokwishafunguliwa mashtaka ni raia saba wa China, raia mmoja wa Bulgaria na Mtanzania mmoja. Tayari zaidi ya Shilingi bilioni 1 zimerejeshwa serikalini, huku kiasi cha Shilingi bilioni 3 kikiwa kimezuiliwa katika akaunti za watuhumiwa, kikisubiri kukamilika kwa uchunguzi.

Nyakizee amewataja waliokamatwa kuwa ni Yao Licong na Wang Weisi, wakazi wa Phoenix Apartments, Oysterbay, Kinondoni, Dar es Salaam. Watuhumiwa hao walikamatwa wakiwa na fedha taslimu Dola za Kimarekani 707,075 sawa na takribani Shilingi 1,732,333,750, pamoja na Shilingi 281,450,000 za Kitanzania, fedha zilizokuwa zimehifadhiwa ndani ya gari kwenye mifuko ya sandarusi.