Aliyekuwa waziri mkuu nchini Kenya Raila Odinga amefariki akiwa na umri wa miaka 80.
Raila amefariki wakati akifanyiwa matibabu katika hospitali moja nchini India kulingana na duru za familia.
Magazeti ya India Mathrubhumi na The Hindu yaliripoti habari hiyo kwa mara ya kwanza Jumatano asubuhi, yakisema Odinga alipatwa na mshtuko wa moyo wakati wa matembezi ya asubuhi katika Hospitali ya Macho ya Sreedhareeyam Ayurvedic na Kituo cha Utafiti, ambako amekuwa akitibiwa kwa siku tano zilizopita.
Msemaji wa kituo hicho aliiambia AFP kwamba Odinga alipata matatizo ya kupumua na kuzimia mwendo wa saa 07:45 asubuhi. Alikimbizwa katika hospitali ya kibinafsi ya karibu, lakini hali yake ilidhoofika.
Odinga ambaye amemwacha mjane na watoto watatu ni mwanasiasa mashauhuri wa Kenya ambaye aliwahi kuwa waziri mkuu wa nchi hiyo kuanzia 2008 hadi 2013.
Kabla ya kifo chake kiongozi huyo atakumbukwa kwa kupigania uhuru wa kidemokrasia, haki za kibinadamu na mabadiliko ya kitaifa.
