Leo naandika makala hii baada ya Taifa kuwa limepata mapigo makubwa mawili. Pigo la kwanza ni vifo vya wanafunzi 32 wa Shule ya Msingi St. Lucky Vincent, walimu wawili na dereva mmoja. Sina hakika siku ya mazishi ya kitaifa ya watoto hao mwenzangu wewe unayesoma makala hii ilikuwaje, ila mimi nilijikutana machozi yananibubujika.
Sitanii, hakika huu umekuwa msiba wa kitaifa. Msiba huu umetuunganisha. Umenikumbusha utu wa Watanzania. Umenikumbusha miaka ya 1978/1979 wakati Tanzania inapigana vita na Uganda. Wazazi wetu ilikuwa wanatufuata shule na kuwaambia walimu watuachie turudi nyumbani huku mizinga ikiwa imechachamaa.
Nakumbuka kulikuwa na kilimo cha chai (amajani) eneo la Rwomunda wakati tunatoka Kyakailabwa, ilikuwa tunaingia na kuigiza vita tukirushiana na kufyatuliana mbegu za majani ya chai (ebimarala). Kwetu sisi mizinga ilikuwa inalia, lakini tunaendelea na mchezo. Nawakumbuka Salvandi Salvatory, Domino, Desmond, Karina na wengine tukiwa katika mchezo huu. Wazazi walikuwa wakituasa mizinga ikilia tuingie kwenye handaki.
Sitanii, sisi tulikuwa tunashangilia mizinga ikipigwa, ila wazazi walikuwa wanatokwa na machozi usipime. Walijua hatari na maana ya kifo. Nakiri vifo vya watoto hawa, vimenikumbusha Vita ya Kagera. Nimepata na kuhisi uchungu waliokuwa wakipata wazazi wetu. Nakumbuka tukisikiliza Sauti ya Ujerumani, akitangaza Sekione Kitojo na Radio Tanzania Dar es Salaam, akitangaza Jacob Tesha.
Kila wakisoma taarifa za habari walisoma salamu za heri kutoka kwa mataifa, makabila na dini mbalimbali za kutiana moyo. Hili ndilo nililoshuhudia wakati wa maziko ya kitaifa ya watoto wa shule ya St. Lucky Vincent. Tuna kawaida na kukubali na kusema Bwana alitoa, Bwana ametwaa, jina la Bwana lihimidiwe, ila tuvuke hapo. Dereva angesikiliza ushauri alioambiwa, watoto hawa wangekuwa hai. Soma habari kuu tuliyoichapisha.
Sitanii, nimeigusia hii ya watoto hawa lakini kimsingi leo nataka kurejea mada niliyoiandika wiki tatu zilizopita juu ya Kodi ya Majengo. Sina shida na kodi hii, ila shida yangu ni aina ya majengo yanayolipishwa. Sheria zote za kodi za hapa Tanzania na za kimataifa, zinataja kuwa msingi wa kulipa kodi ni kupata mapato. Huwezi kulipa kodi kwa fedha ambazo hujapata/hujapokea.
Mheshimiwa Rais John Pombe Magufuli, katika hili naomba kukushirikisha. Yapo mataifa ambayo hayatozi kodi ya majengo. Kuwait, Israel, Falme za Kiarabu ni baadhi ya mifano michache tu ya nchi zisizotoza Kodi ya Majengo. Katika sheria tuna kanuni ya Kilatini tunayoiita “Quicquid plantatur solo, solo cedit”.
Kanuni hii inamaanisha kuwa kila kilichoshika kwenye udongo ni sehemu ya udongo.
Kwa mantiki hiyo, kwa nchi ambazo mfumo wa kodi ardhi inamilikiwa na Serikali (kama ilivyo Tanzania) wananchi hukodisha ardhi na  ndiyo maana hudaiwa kodi ya ardhi. Kodi hii ikiishalipwa, inahalalisha umiliki wa muda wa kiwanja husika. Kutoza Kodi ya Majengo maana yake ni kuitoza ardhi kodi mara mbili ikiwa majengo haya hayafanyi biashara.
Kichwa cha makala hii kinamwomba Rais John Magufuli kumuuliza Rais (mstaafu) Benjamin Mkapa juu ya masuala ya kodi. Mwezi Juni, mwaka 2005 nilikuwa kwenye ukumbi wa Bunge Dodoma, wakati bajeti ya Serikali inasomwa. Aliyekuwa Waziri wa Fedha, Basil Pesambili Mramba, alifuta iliyoitwa kodi ya kichwa. Kodi hii ilikuwa Sh 3,000 kwa kila mwanaume mwenye umri wa miaka 18 na kuendelea.
Hadi kodi hii inalipwa, watu walikuwa wanaishi maporini. Leo Kodi ya Majengo inatozwa kati ya Sh 10,000 na 20,000 kulingana na mkoa au manispaa walivyoamua madiwani. Kiasi hiki ni mara tatu hadi saba ya kodi ya Sh 3,000 iliyojulikana kama Kodi ya Maendeleo (Kodi ya Kichwa) iliyofutwa mwaka 2005. Watendaji wanasema kodi hii ni kidogo, lakini nakumbusha kuwa watu walikuwa wanalala misituni.
Nimesikiliza, kwa mfano, Halmashauri ya Manispaa ya Ilala inatakiwa kukusanya Sh bilioni 18 kwa mwaka. Binafsi nitawahi kulipa maana, hasa kwa kuandika makala hii wanaweza kunitolea mfano. Mheshimiwa Rais, mtu akijenga nyumba yake inakuwa ni mali yake. Kumtaka alipe kodi isiyo na ukomo, kwa maana ya Kodi ya Majengo ya kila mwaka, ni kumgeuza mpangaji katika nyumba aliyojenga kwa fedha zake.
Sitanii, maneno matamu yanatumika kuwa kodi hii haina madhara ni ya hiyari. Wananchi msidanganyike. Huko Pennsylvania, Marekani, watu wapatao 10,000 nyumba zao zinauzwa kila mwaka kwa kukosa kodi ya majengo. Kitu kinachoitwa ‘kodi’ tusikichezee. Watu wanadhani ni wamiliki wa magari, kwa mfano, wakati uhalisia hata ukinunua gari mmiliki halisi ni Serikali. Ukitaka kujua wewe si mmiliki wa gari hilo, basi pitisha miaka mitatu bila kulipa ‘road license’ uone kama gari lako halitanadishwa!
Naomba kuhitimisha makala hii kwa kusema wenye nyumba za biashara walipe kodi kwa maana wanaingiza pato, ila wenye nyumba za kuishi, kuna watu nyumba zao zitauzwa ikiwa watatakiwa kulipa kodi. Kuna umaskini wa kutisha kwenye jamii. Kama wanaume walilala misituni kwa Sh 3,000 kwa mwaka, naaminni 10,000 au 20,000 itauza nyumba za watu au kuwafanya wajinyonge. Kodi hii iangaliwe upya. Zilipe nyumba za biashara na si nyumba za makazi. Mungu ibariki Tanzania.

By Jamhuri