Na Mwandishi Wetu
Rais Mstaafu, Jakaya Kikwete ameongoza Mkutano wa Bodi ya Taasisi ya Ubia wa Elimu Duniani (Global Partnership for Education, GPE), ambaye yeye ni Mwenyekiti wake.
Mkutano huo unaofanyika Paris, Ufaransa tarehe 3-4 Juni, 2025 unahudhuriwa na Wajumbe zaidi ya 40 wanaowakilisha makundi mbalimbali ya Ubia huo ambao wanatoka nchi 7 tajiri zaidi duniani (G7), nchi washirika kutoka kanda zinazoendelea kiuchumi, hususan zilizopo Afrika na Asia, pamoja na Mashirika mbalimbali ya kimataifa.

Pamoja na mambo mengine, Mkutano huo wa Bodi umejadili namna Taasisi ya GPE inavyoweza kuhimili mabadiliko yanayotokea duniani kwa sasa, hususan kufuatia sintofahamu iliyosababishwa na mabadiliko ya kimtizamo ya Serikali ya sasa ya Marekani chini ya Rais Donald Trump. Kama ilivyo kwa Taasisi na Mashirika mengine ya Kimataifa, GPE inatarajiwa kuathiriwa na mabadiliko hayo.
Taasisi ya GPE iliyoanzishwa na nchi zenye uchumi mkubwa duniani (G7) imeendelea kutoa mchango mkubwa katika maendeleo ya Elimu duniani kwa kusaidia kutimiza lengo la 4 la Maendeleo Endelevu la Umoja wa Mataifa la kumpatia kila mtoto elimu bora, yenye usawa na kutoa fursa kwa wote kujiendeleza.
GPE imejikita kutekeleza miradi yake katika nchi zinazoendelea na nchi masikini zaidi duniani, hususan zile zinazokabiliwa na changamoto kama vile vita, athari za mabadiliko ya tabianchi, nk.
Hadi sasa takriban watoto milioni 860 duniani kote wamenufaika na ufadhili unaotolewa au kuratibiwa na Taasisi ya GPE. Katika kipindi hiki cha mpito, GPE imenuia kuimarisha mfumo wake wa kufanya ubia na wadau mbalimbali wa kimaendeleo duniani ili kudumisha na kupanua zaidi ufadhili wa miradi yake.

Wachambuzi wameeleza kuwa uchumi wa dunia na nchi unapoyumba, moja ya sekta ambazo huwa za kwanza kuathirika zaidi ni sekta ya elimu.
Hadi kufikia mwaka 2030, GPE imelenga kuwafikia na kusaidia watoto takriban milioni 100 zaidi duniani kote wanaokosa elimu yenye ubora au wanaosoma na kujifunzia katika mazingira magumu.
Pembezoni mwa Mkutano huo wa Bodi, Rais Mstaafu Kikwete alipata pia fursa ya kukutana na kufanya kikao na Waziri anayeshughulikia Ubia wa Kimataifa na Nchi zinazozungumza Kifaransa Thani Mohamed-Soilihi ambapo pamoja na mambo mengine walijadili namna ya kukuza zaidi ushirikiano kati ya Taasisi ya GPE na Ufaransa.
Kikao hicho kilihudhuriwa pia na Balozi wa Tanzania nchini Ufaransa, Ali Jabir Mwadini, ambaye alitumia fursa hiyo kuishukuru Serikali ya Ufaransa kwa ushirikiano mzuri uliopo kati ya Tanzania na Ufaransa na kueleza utayari wa Tanzania kudumisha na kukuza zaidi mahusiano hayo.




