RAIS Mstaafu wa Jamhuri ya Msumbiji, Filipe Jacinto Nyusi amewasili hapa nchini katika Mkoa wa Mtwara
kwa ajili ya kuelekea Lupaso wilayani Masasi kwenye Kumbukizi ya kifo cha aliyekuwa Rais wa awamu ya tatu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania hayati Benjamin William Mkapa inayotarajiwa kufanyika Julai 23, 2025.

Akizungumza baada ya kuwasili, Rais huyo Mstaafu wa nchi hiyo ya Msumbiji amesema kwa kiasi kikubwa walikuwa wanaelewana na aliyekuwa Rais wa tatu Benjamini Mkapa.

“Mama Mkapa aliponifahamisha nikasema hilo mama mimi siyo lazima kuniita wewe ungenifahamisha tu, huwezi kumwalika mtu kuja kwenye shughuli kama hii hapa tumekuja kwenye sherehe ya maisha ya mzee wetu na tulikuwa tunaelewana sana na mzee,”amesema Nyusi.

Amesema mpaka kufukia hatua hiyo kwa sasa wako pamoja na watajumuika wote na kikamilifu katika tukio hilo.

Amesema hapo awali hapa nchini walikuwa na hospitali kubwa iliyokuwa ikiitwa Flerimo ambapo wakati huo yeye alikuwa kijana kwahiyo amefika nyumbani.

Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Kanali Patrick Sawala amemuhakikishia Rais huyo Mstaafu wa Jamhuri ya Msumbiji kuwa Mtwara ni salama na wananchi wanaendelea vizuri na shughuli zao za kiuchumi. 

“Tumefarijika sana tulipopata taarifa kwamba utakuja kuungana nasi na familia hii ya mzee wetu hayati Benjamin William Mkapa katika tukio la kesho (Julai 23, 2025) ambalo litafanyika kule Masasi”amesema Sawala

Aliongeza kuwa” Kwahiyo tumefarijika sana kukuona kiongozi wetu, kwetu sisi huku wanamtwara tuko kusini kabisa tunapakana kabisa na Mozambiki, taratibu, tamaduni zetu lakini shughuli za kiuchumi misimu inafanana”amesisitiza Sawala.