Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amesema Serikali itaendelea na ujenzi wa masoko ya kisasa katika maeneo mbalimbali ya Zanzibar kwa lengo la kuwawezesha wafanyabiashara kufanya shughuli zao katika mazingira bora, salama na yenye hadhi.
Rais Dkt. Mwinyi ameyasema hayo leo tarehe 4 Januari 2026 alipolizindua Soko la Kisasa la Mbogamboga la Mombasa, lililopo Mkoa wa Mjini Magharibi.

Ameeleza kuwa Serikali inapowahamisha wafanyabiashara kutoka maeneo yao ya awali, hufanya hivyo kwa nia njema ya kujenga masoko yenye viwango na hadhi, pamoja na kuwaandalia mazingira mazuri yatakayochangia ukuaji wa biashara zao na ustawi wa maisha yao.
Rais Dkt. Mwinyi amewahakikishia wananchi kuwa Serikali ipo katika maandalizi ya kujenga soko kubwa na la kisasa katika eneo la Kibanda Maiti, pamoja na uanzishaji wa Bazaar katika Mtaa wa Kwa Hajitumbo, Wilaya ya Mjini, hatua itakayosaidia kudhibiti biashara holela, kuondoa mazingira duni katika masoko na kuzuia ufanyaji wa biashara pembezoni mwa barabara.
Aidha, amesema Serikali itaendelea kutoa mikopo isiyo na riba kwa wafanyabiashara ili kuwawezesha kukuza mitaji yao, huku akitoa wito kwa watakaopewa fursa ya kuliendesha soko hilo jipya kuhakikisha wanalinda miundombinu na kuimarisha usafi wakati wote.

Rais Dkt. Mwinyi ametoa maelekezo maalum kwamba wafanyabiashara wa mwanzo waliopisha ujenzi wa Soko la Mombasa wapewe kipaumbele wakati wa ugawaji wa vizimba vya kufanyia biashara sokoni hapo.
Vilevile, ameushauri Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (ZSSF) kujikita zaidi katika uwekezaji wa miradi mikubwa yenye tija, ikiwemo nishati ya umeme, teksi za baharini na mabasi ya umeme, kufuatia mafanikio yaliyopatikana katika miradi ya nyumba za Makaazi na Masoko.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii Zanzibar (ZSSF), Ndugu Nassor Shaaban, ameishukuru Serikali kwa kuendelea kuiamini taasisi hiyo katika utekelezaji wa miradi ya uwekezaji inayochangia ukuaji wa uchumi na maendeleo ya Zanzibar, ikiwemo ujenzi wa nyumba za Makaazi na Masoko ya kisasa.
Ujenzi wa Soko la Kisasa la Mbogamboga la Mombasa umegharimu jumla ya Shilingi Bilioni 16.6, na umetekelezwa na Kampuni ya RANS.






