RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, amesema Zanzibar imepiga hatua kubwa kulinda haki za wanawake kwa kuwa na sera na sheria bora zinazohakikisha usalama, usawa wa kijinsia na kuwepo kwa miji na maeneo salama ya kijamii.

Dk. Mwinyi, aliyasema hayo wakati akifungua mkutano wa saba wa dunia wa viongozi wa miji na maeneo salama kwa jamii uliofanyika katika hoteli ya Madinat Al- Bahr Mazizini.

Alisema serikali imekuwa mstari wa mbele kuimarisha usalama wa maeneo ya umma na kutokomeza ukatili wa kijinsia kupitia sera madhubuti na utekelezaji wa mikakati maalum.

Aidha alisema mkutano huo ulioandaliwa kwa ushirikiano na UN Women, unaakisi jitihada za kimataifa za kujenga jamii salama kwa wote, hasa wanawake na wasichana kupitia utekelezaji mzuri wa sera na sheria zinazohakikisha fursa na ustawi wao.

Rais Mwinyi alibainisha kuwa Zanzibar imepiga hatua katika kuhakiksha usalama wa miji ambao umegusia ujumuishwaji wa wanawake na wasichana katika utekelezaji wa sera na sheria za nchi.

“Safari ya maendeleo ya Zanzibar inalenga mabadiliko ya kijamii kupitia ajenda ya Dira ya Maendeleo ya Zanzibar ya 2050, usalama na usawa wa kijinsia ni nguzo kuu za mafanikio haya,” alisema Rais Mwinyi.

Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Riziki Pembe Juma akizungumza katika mkutano wa saba wa dunia wa viongozi wa miji na maeneo salama kwa jamii, uliofanyika katika hoteli ya Madinat Al- Bahr Mazizini, Unguja

Hata hivyo alisema serikali imetenga fedha mahsusi za kusimamia usalama wa wanawake, wasichana na watoto, sambamba na kuunda kamati za kitaifa zinazoshughulikia masuala hayo kwa ushirikiano na wadau mbalimbali wa maendeleo.

Alibainisha kuwa bila usalama wa watu wote, maendeleo hayawezi kuwa endelevu na kuamini kuwa usalama ni haki ya kila mtu na si suala la anasa au hiyari.

“Tunaamini kuwa hakuna maendeleo ya kweli bila jamii yenye amani, usalama na haki, miji salama ni sehemu ya mikakati yetu ya muda mrefu ya kuhakikisha ushirikishwaji na ustawi wa wote,” alisisitiza.

Alifahamisha kuwa Zanzibar imekuwa ni nchi salama na watu wanafanya majukumu yao bila kubugudhiwa hata katika kuelekea kipindi cha uchanguzi.

Aliahidi kuwa serikali itaendelea kuweka mikakati ya kuimarisha usawa wa kijinsia na kuondoa unyanyasaji wa kijinsia na kuwawezesha wanawake kiuchumi.

Dk. Mwinyi ameipongeza taasisi ya UN Women kwa mikakati na juhudi zake kuhakikisha wanawake duniani kote wanalindwa dhidi ya vitendo vya udhalilishaji.

Alizitaka taasisi za kikanda na za kimataifa kuungana pamoja kwa lengo la kuendeleza miji na maeneo salama na rafiki kwa maendeleo ya wanawake.

Naye Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa, Serikali za Mitaa na Idara Maalum za SMZ, Masoud Ali Mohammed, alisema Zanzibar imechaguliwa kwa heshima kuwa mwenyeji wa mkutano huo kutokana na juhudi zake katika kulinda haki za wanawake na usalama wa miji.

Alisema hayo yote yametokana na uongozi imara na wenye kujali amani na utulivu kwa watu wake unaoongozwa na Dk. Hussein Ali Mwinyi.

Mapema Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsi, Wazee na Watoto, Riziki Pembe Juma, alisema Zanzibar ina sera imara katika masuala ya jinsia pamoja na utekelezaji wake ikiwemo sera ya jinsia ya mwaka 2017, sera ya hifadhi ya jamii ya mwaka 2018 na sheria ya mtoto nambari 6 ya mwaka 2011.

Sheria nyengine alisema ni ya kulinda mwari na mtoto wa mzazi mmoja na sheria nyengine mbalimbi ambazo zote hizo zimelenga kusimamia usawa wa kijinsia na ustawi wa kamii katika nchi.

Zainab Katimba ni Naibu Waziri, TAMISEMI Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, alisisitiza kuwa usalama katika maeneo ya umma hauwezi kutenganishwa na dhana ya usawa wa kijinsia.

Alisema jamii salama ni ile inayolinda wanawake na kuwashirikisha kikamilifu katika shughuli za kijamii, kiuchumi na kisiasa.

“Ni jukumu la kila mmoja kuhakikisha udhalilishaji wa kijinsia unakomeshwa na miji salama inapatikana kwa wote kwani usalama wa wanawake ni msingi wa maendeleo ya jamii,” alisema.

Mstahiki Meya wa Jiji la Zanzibar, Mahmoud Mohamed Mussa, ni wajibu kulinda maadili ya jadi na kutumia utamaduni wa amani kama daraja la kujenga miji jumuishi.

Mratibu kutoka UN Women, Susan Ngogi Namondo, alisema wanawake wanakumbana na changamoto nyingi katika miji, hasa ukatili wa kijinsia, na ndio sababu ya mkutano huo kuwepo kama jukwaa la kutafuta suluhisho la pamoja.

“Miji jumuishi na salama imeongeza ushirikiano na ushirikishwaji wa wanawake katika nyanja mbalimbali za maendeleo na Zanzibar ni mfano wa eneo lenye amani na mazingira bora ya kuwawezesha wanawake,” alisema.

Alisema zaidi ya asilimia 20 ya wanawake nchini Tanzania wanakumbwa na ukatili wa kijinsia hali inayokwamisha maendeleo yao.

Alisema ni wajibu wa kila taifa kuunganisha nguvu na kuweka sera thabiti za kulinda wanawake.