Rais wa Kenya William Ruto ameagiza kupelekwa mara moja kwa kikosi cha dharura kutoka taasisi mbalimbali kusaidia juhudi za uokoaji kufuatia mafuriko ya ghafla yaliyosababisha vifo kadhaa katika jiji kuu la Nairobi.
Mamlaka zinasema watu 25 wamefariki dunia baada ya mvua kubwa kunyesha na kusababisha mafuriko katika maeneo mbalimbali ya jiji hilo.
Mapema Jumamosi, wahudumu wa misaada walionekana wakitoa miili ya watu kutoka kwenye maji katika sehemu tofauti za Nairobi baada ya mvua hizo kubwa.
Mafuriko yalizoa makumi ya magari, baadhi ya nyumba na pia kuathiri safari za ndege katika uwanja mkubwa wa ndege wa Afrika Mashariki, Jomo Kenyatta.
Shirika la ndege la Kenya Airways lilitangaza kwenye ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa X kwamba baadhi ya safari za ndege zililazimika kubadilisha uelekeo wa safari kutoka Nairobi kwenda mji wa pwani wa Mombasa kutokana na mvua hizo.
Kwa mujibu wa shirika la msalaba mwekundu la Kenya, mbali na Nairobi, mafuriko pia yameripotiwa katika kaunti ya Kisumu baada ya mto kufurika na kuvunja kingo zake.
Jumla ya kaya 381 zimeathirika, huku nyumba na mashamba yakifunikwa na maji.
Wakati huo huo, Idara ya hali ya hewa ya Kenya imetabiri kuwa mvua kubwa zitaendelea kunyesha mwishoni mwa wiki hii.
Ripoti ya mwaka 2024 kutoka taasisi ya kimataifa inayofuatilia mabadiliko ya tabia nchi imebaini kuwa ongezeko la joto duniani linachangia kiwango cha mvua kuwa kikubwa katika ukanda wa Afrika Mashariki, hali inayosababisha mafuriko wakati wa msimu wa mvua kuwa mara mbili zaidi ya hapo awali.

