Rais wa Kenya William Ruto amesema anajenga kanisa katika Ikulu jijini Nairobi ambalo atagharamia mwenyewe – na kuongeza kuwa hana sababu yoyote ya kuomba msamaha.

“Sitamwomba mtu yeyote msamaha kwa kujenga kanisa. Shetani anaweza kuwa na hasira na anaweza kufanya anachotaka,” alisema.

Kauli hiyo pekee imewakasirisha Wakenya ambao tayari wamekatishwa tamaa na mtindo wake wa uongozi na kile wanachokichukulia kama mtego wa serikali na kanisa.

Haijabainika ni nani Ruto alikuwa akimtaja kama “shetani” katika maoni yake katika Ikulu, lakini anasema hakuna kitakachozuia mradi huo kuendelea.

“Sikuanza kujenga kanisa hili nilipoingia Ikulu. Nilikuta kanisa lipo lakini limejengwa kwa mabati. Je, hilo linaonekana kufaa kwa Ikulu?” Ruto aliwaambia wanasiasa kwenye mkutano alioandaa Ijumaa.

Siku ya Ijumaa, moja ya magazeti mashuhuri nchini Kenya, Daily Nation, lilichapisha miundo ya usanifu inayoonyesha jengo kubwa lenye madirisha ya vioo na uwezo wa kuhudumia watu 8,000.

Jarida hilo lilihoji iwapo mradi huo unaendana na katiba ya ya Kenya.

Pia kumekuwa na ukosoaji wa gharama hiyo, inayokadiriwa kufikia $9m (£6.5m), wakati ambapo Wakenya wengi wanatatizika na kupanda kwa gharama ya maisha.

Ruto alisema atalipia kanisa hilo kutoka mfukoni mwake, hata hivyo hilo linazua swali iwapo ana haki ya kujenga jengo hilo kubwa kwenye mali ya serikali.